Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Obadia Bwegoge jana tarehe 25 Machi, 2025 alifanya ukaguzi wa kikazi katika Gereza la Mahabusu Mkuza na Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha.
Akipokea taarifa ya Gereza la Mahabusu Mkuza iliyosomwa na Mkuu wa Gereza hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Ibrahim Nyamka alisema kutawanyika kwa Mahakama kunasababisha kushindwa kuwafikisha Mahabusu mahakamani kwa wakati.
Licha ya kwamba kwa sasa kuna basi kwa ajili ya kusafirishia mahabusu bado mtawanyiko wa Mahakama umekuwa changamoto, Mkuu huyo wa Gereza alisema kuwa, kutokana na changamoto hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha vijijini umeahidi kutoa eneo la hekari 60 kwa ajili ya ujenzi wa Gereza ambapo baada ya kukamilika kwa ujenzi huo kutaondoa changamoto ya umbali wa Mahakama mfano Mahakama ya Mwanzo Magindu na Soga ambazo ziko pembezoni kijiografia ambapo umbali wake umekadiriwa kuwa kilometa zaidi ya 50.
SSP Nyamka alisema katika kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusiana na kuachana na matumizi ya kuni (nishati chafu) na kutumia nishati safi, Gereza hilo limeanza matumizi ya nishati safi kwa kutumia makaa ya mawe huku wakiendelea na mchakato wa matumizi ya gesi.
Katika ukaguzi huo, Jaji Bwegoge alikutana na wafungwa na mahabusu wa Gereza hilo na kupokea changamoto mbalimbali na kuzitatua, changamoto hizo ni pamoja na kutoleta mashahidi kwa wakati, washtakiwa kufutiwa mashauri na kukamatwa tena na pia kuchelewa kusikilizwa kunasababisha mahabusu kukaa kwa muda mrefu.
Akijibu changamoto hizo, kuhusu suala la kufutiwa shauri na kukamatwa tena, Mhe. Bwegoge alisema shauri likifutwa likarudishwa inabidi upelelezi uwe umekamilika na lianze kusikilizwa mara moja na kama litakuwa kwa Hakimu mwingine ni jukumu la mshtakiwa kumwambia Hakimu kwamba shauri hilo lilifutwa na sasa limeletwa tena ili Hakimu husika aweze kuchukua hatua.
“Kama itafutwa kesi kwa sababu shahidi hajaja mahakamani kwa hiyo siku anarudishwa mahakamani lazima awe na shahidi mlangoni kama ikienda ndivyo sivyo na wewe unaweza kukumbusha utaratibu huo,” alisema Jaji Bwegoge.
Pamoja na kuzungumza na wafungwa na mahabusu, Mhe. Bwegoge alifanya ukaguzi maeneo mbalimbali ya gereza hilo ikiwemo jikoni na kwenye mabweni ya wafungwa na mahabusu.
Kadhalika, Mhe. Bwegoge alifanya ukaguzi pia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha na kuona namna ambavyo kazi ya usikilizwaji wa mashauri inavyofanyika.
Baada ya ukaguzi huo, Jaji Bwegoge alifanya mazungumzo na watumishi wa kada mbalimbali katika Mahakama hizo na kuwapongeza watumishi kwa utendaji kazi na mazingira kutokana na kwamba hakuna changamoto nyingi ambazo zinaashiria vinginevyo, na pia amewakumbusha kuendelea kuwajibika kama ilivyo ada.
Mhe. Bwegoge aliwakumbusha watumishi kuwa, taswira ya Mahakama inatokana na namna wanavyowahudumia wananchi. Amewakumbusha kwamba vile wanavyowahudumia wateja ni ndivyo wanavyochukulia sura ya Mahakama ilivyo.
Aliwataka watumishi pia kuepuka kuzunguka na kupiga hadithi na wateja hata kama wanafahamiana ili kuondoa wasiwasi kwa upande wa pili, ili wajue kwamba wateja wote kwa usawa bila kuegamia upande wowote. Amewataka watumishi hao kuweka imani kwa wateja ili wasiwashuku kwa lolote.
Aidha, Jaji Bwegoge alisema kwamba Mahakama ya miaka 12 iliyopita sio Mahakama ya sasa siku zinakwenda na mazingira ya Mahakama yamebadilika, kwakuwa huko nyuma mazingira hayakuwa rafiki kama sasa hivyo amewataka watumishi hao kuendelea kuishi kwa matumaini.
Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe.Aziza Mbadjo aliwapongeza watumishi wa Mahakama hizo kwa kufanya kazi kwa utaratibu na kutokuwa na kashfa yoyote na kwamba siku zote wamekuwa wafuata maelekezo ya viongozi na usikivu wa watumishi hao.
Aidha, Mhe. Mbadjo amemueleza Jaji Bwegoge kuwa, amefanya ukaguzi na kukuta vitu vimepangwa vizuri huku akitoa mfano wa stoo ya vielelezo ambapo alisema stoo hiyo ina vielelezo vya Mahakama zote mbili vilivyopangwa vizuri. Amekagua pia mifumo yote na kudai iko vizuri licha ya changamoto ndogondogo za kibinadamu.
Naye, Afisa Tawala wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Lucy Tirukaizile alifanya ukaguzi kwenye mifumo ya PEPMIS na Ofisi Mtandao ‘e-Office’ na kubainisha kuwa iko vizuri na kuwasihi Watumishi wa Mahakama hizo kufanya kazi kwa bidii na kujiendeleza kielimu kwani elimu haina mwisho.
Katika ukaguzi huo Jaji Bwegoge aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo, Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Suda Mbilinyi na Afisa Tawala wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Lucy Tirukaizile.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni