Jumatano, 26 Machi 2025

JAJI MFAWIDHI SHINYANGA AMTAKA MKANDARASI KUMALIZA MIRADI YA UJENZI KWA WAKATI

Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama-Simiyu

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe.Frank Mahimbali amemtaka Mkandarasi ‘Skywards Ltd’ anayetekeleza miradi ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo Nyalikungu Maswa, Lagangabilili Itilima na Mhango Bariadi kuhakikisha wanakamilisha miradi ya ujenzi wa Mahakama hizo kwa muda uliopangwa bila nyongeza ya muda wa ziada.

Mhe. Mahimbali aliyasema hayo jana tarehe 25 Machi, 2025 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Mahakama hizo na kumuhimiza Mkandarasi kukimbizana na muda uliobaki ili wananchi katika maeneo hayo waanze kupata huduma katika majengo hayo.

“Ni muhimu sana kukamilisha miradi hii na kuutumia vizuri muda uliobaki kukamilisha shughuli zote kwenye miradi hii, kwani wananchi wanahitaji kuanza kupata huduma katika majengo haya,’’ alisema Jaji Mahimbali.

Kwa mwaka huu wa fedha Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imepata jumla ya miradi mitano ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo inayotekelezwa katika Wilaya za Shinyanga, Kahama, Maswa, Bariadi na Itilima na miradi yote ilianza kutekelezwa mwezi Agosti, 2024 na inatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2025.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mahimbali aliwataka Watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga wanaopata fursa ya kuhudhuria mafunzo, wanaporejea katika vituo vyao wahakikishe wanawapatia elimu waliyoipata watumishi waliobaki vituoni ili kuwa na uelewa wa pamoja. Aliwahimiza pia watumishi wa Mahakama katika Kanda hiyo, kuhakikisha wanapata fursa ya kujiendeleza kielimu kila wanapopata fursa. 

Jaji Mahimbali anaendelea na ziara ya ukaguzi wa kawaida wa Mahakama unaofanyika kila robo mwaka ambapo hadi kufikia jana alikuwa ameshatembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mahakama za Wilaya Maswa, Bariadi, Itilima na Busega. Aidha, ziara ya ukaguzi inaendelea kwa Mahakama zilizobaki ambazo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mahakama za Wilaya Shinyanga, Kahama, Kishapu na Busega.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe Frank Mahimbali (kulia) akipokea maelezo ya mradi kutoka kwa Mhandisi Alex Silas (wa pili kulia) wakati akikagua ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Nyalikungu-Maswa jana tarehe 25 Machi, 2025.

Mkadiriaji Ujenzi QS Edson Minata akitoa maelezo ya Mradi wa Mahakama ya Mwanzo Lagangabilili-Itilima kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga (hayupo katika picha) wakati alipotembelea jana tarehe 25 Machi, 2025 kufahamu maendeleo ya mradi huo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (kushoto) akisisitiza jambo wakati alipofanya ukaguzi wa Mradi wa Mahakama ya Mwanzo Lagangabilili- Itilima jana tarehe 25 Machi, 2025.

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita akifafanua jambo wakati Jaji Mahimbali alipotembelea Mradi wa Mahakama ya Mwanzo Lagangabilili-Itilima.

Muonekano wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Lagangabilili- Itilima ambalo lipo katika hatua ya upauaji kwa sasa.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (wa tano kulia) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Meatu.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni