- .
Na. ALLY. RAMADHANI -Mahakama, Katavi
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha, ameitaka Mkandarasi wa Kampuni ya M/s AZHAR Construction Co. Ltd kukamilisha ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC), Katavi kinachoendelea kujengwa katika Mkoani Katavi kwa wakati na kuzingatia viwango na ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa mkataba.
Bw. Magacha ametoa maelekezo hayo mahsusi tarehe 25 Machi, 2025 kwa ajili ya kukagua shughuli zinazoendelea katika mradi wa ujenzi wa Kituo hicho.
Akitoa maelekezo kwa mkandarasi wa mradi huo, Mtendaji wa huyo alisisitiza kuwa ni muhimu kwa mkandarasi huyo kuongeza vifaa (vilivyopungua ili kusaidia kukamilika kwa mradi huo ndani ya muda.
Aidha, Magacha amesema hayo baada ya kugundua changamoto zinazosababisha kusuasua kwa mradi huo, katika kikao kinachohusu ujenzi huo.
“Tupo tayari kutumia aina yeyote ya rasilimali iwe fedha, nguvu kazi, na muda yani usiku na mchana ili kabla ya kuvuka kwa nusu ya mwezi Juni mwaka huu mradi wa ujenzi huu uwe tayari umekamilika,” anasema Magacha.
Naye Meneja Mradi wa ujenzi huo, Msanifu Linda Kasilima alitoa ushauri kwa mkandarasi kuongeza nguvu kazi watu ili kuharakisha mradi huo, ambapo wazo hilo liliridhiwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo,Mhandisi Shabani Kapinga ambaye ndiye Mkandarasi.
“…tayari kuna idadi ya nguvu kazi watu tunategemea iongezeke kuanzia kesho kutoka sehemu tofauti tofauti ndani ya Mkoa wa Katavi na nje ya mkoa,” amesema Kapinga.
Pia timu ya Wahandisi kutoka upande wa Mahakama ya Tanzania, baada ya kikao hicho kilichofanyika kwa zaidi ya masaa matano walipata wasaa wa kutembelea jengo na kuangalia shughuli zinazoendelea.
Aidha akiwa katika eneo la mradi wa ujenzi wa Kituo hicho,Mtendaji wa huyo alipata wasaa wa kusalimiana na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi.
Akihitimisha kikao chake na wakandarasi hao, amewataka kuzingatia kalenda ya shughuli zilizopangwa kufanyika kwa kipindi cha utekelezaji wa mkataba pamoja na ubora wa vifaa vinayonunuliwa, na kusisitiza kwamba vifaa vyote viwepo tayari na hiyo idadi ya nguvu kazi watu iwe tayari.
Moja ya nguzo katika Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ni Utoaji Haki kwa wakati. Mahakama inatekeleza mpango huu kwa kuboresha mazingira ya utoaji haki na kusogeza huduma za utoaji haki kwa wananchi kwa kujenga miundombinu bora na wezeshi itakayochangia ufanisi mzuri wa utekelezaji wa nguzo hii.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leornad Magacha akisalimiana na baadhi ya watumishi wa Mahakama Mkoa wa Katavi.
Wataalamu kutoka upande wa Mahakama, wakikagua shughuli zinazoendelea katika mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachoendelea kujengwa.
Masanifu wa ujenzi huo, Bi. Linda Kasilima, ambaye pia ni Meneja wa Mradi huo akizungumza kwenye kikao cha usimamizi wa miradi, wakati wa ukaguzi wa shughuli zinazoendelea katika mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachoendelea kujengwa mkoani Katavi.
(Habari hii imehaririwa na MAGRETH KINABO- Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni