Na HUBERT MAANGA-Mahakama, Mtwara
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki, hivi karibuni aliungana
na Watumishi kutoka Kanda hiyo kutembelea Kituo cha Elimu ya Watoto wenye
mahitaji maalumu na changamoto mbalimbali, ikiwemo usonji, kilichopo Mtwara
mjini.
Watoto wa Kituo hicho
kinachoitwa ‘Upendo Rehabilitation Day Center,’ wakiongozwa na Walezi wao, waliwapokea
wageni wao kwa furaha na kuwakaribisha.
Baada ya hapo, Jaji
Mfawidhi alizungumza machache na Msimamizi wa Kituo hicho kuhusu watoto na
uendeshaji wake kwa ujumla. Mhe Kakolaki aliwashukuru Walezi wa watoto hao kwa
kazi ya kipekee ya kuwalea na kuwafunza.
"Hawa ni watoto wetu
na wanahitaji msaada na uangalifu maalumu, ninawaomba wasiwe na wasiwasi, bali
waendelee kuwaongoza na kuwatunza. Endeleeni juhudi hii ya upendo kwani mnajaza
moyo wa matumaini,’ alisema.
Jaji Mfawidhi aliwaeleza
Walezi hao kuwa kila wanachokifanya kwa watoto hao ni kikubwa na dhamana kubwa
ya kibinadamu ambayo Mungu atawabariki. Pia aliwasihi Watumishi wenzake kutokuishia
hapo, bali waendelee kuwasaidia na kuwatia nguvu wenzao katika kuwalea watoto hao.
Vile vile, Mhe. Kakolaki
alishirikiana na Watumishi wa Mahakama kuwawezesha watoto hao baadhi ya
mahitaji kama vyakula na vifaa vya kuwasaidia, akitambua changamoto
zinazowakabili.
Alihimiza jamii yote
kushiriki katika kulinda na kuendeleza haki kwani ni Kituo kinachoendelea
kukuza matumaini kwa watoto wenye mahitaji maalum na changamoto mbalimbali.
Baada ya shughuli hiyo matendo
ya hisani, Watumishi wa Mahakama na Wadau mbalimbali walikutana katika Iftar ya
pamoja iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu Mtwara. Iftar hiyo ilikuwa
sehemu ya kukuza ukaribu na upendo, hasa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa
Ramdhan na Kwaresma.
Wakati wa hafla hiyo,
Jaji Mfawidhi aliwasihi Watumishi wote kuendelea kujisogeza kwa Mwenyezi Mungu
na kufanya matendo mema.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Sheikh Jamaldin Chamwi, ambaye alikuwa miongoni mwa Viongozi wa Dini waliohudhuria, alisisitiza ibada na kukazia juu ya yale aliyoyataja Jaji Mfawidhi kabla ya kafunga kwa dua.
Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Mtwara wakishuhudia uchangamfu na ukarimu kutoka kwa watoto.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki akizungumza na watoto, wakionyesha tabasamu na kumfurahia.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki akitoa neno katika Iftar iliofanyika kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu Mtwara.
Majaji wakiwa kwenye meza moja na Viongozi wa Dini wakati wa Iftar.
Watumishi na Wadau mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ya Iftar (juu na chini).
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni