Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Venance Mwakapeje amefanya ukaguzi wa kwanza kwa mwaka 2025 tarehe 25 Machi, 2025 katika Mahakama ya Wilaya Chato na Mahakama za Mwanzo wilayani hapo kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama, kukutana na watumishi kusikiliza na kutatua changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Jaji Mwakapeje amefanya ziara hiyo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi Mhe. Kevin David Mhina wa Mahakama hiyo, ambapo aliongozana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Fredrick Rutashobya Lukuna na Mtendaji wa Mahakama hiyo Bi. Masalu Cosmas Kisasila.
Pia Mhe. Jaji Mwakapeje alikagua Mahakama ya Mwanzo Muganza, Bwanga, Buseresere, Chato Mjini na Mahakama ya Wilaya ya Chato.
Vile vile ziara hiyo ilihusisha kutembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Muganza ili kujionea maendeleo yake.
Aidha, Mhe. Jaji Mwakapeje akiwa na viongozi wengine walisikitishwa na kusuasua kwa maendeleo ya ujenzi huo kwani ulikuwa umesimama na hakuna kilichokuwa kinaendelea likiwa limefikia kwenye hatua ya linta.
Wakati wa kikao pamoja na watumishi wa Mahakama za Wilaya hiyo, Mhe. Jaji Mwakapeje aliwapongeza kwa kazi nzuri walioionesha katika mwaka 2024 kwa kumaliza mashauri ndani ya wakati, ikiwemo kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uendeshaji wa mashauri.
Aidha, Mhe. Jaji Mwakapeje amewaasa watumishi kuzingatia sana suala la maadili kwani ndiyo wa mgongo wa Mahakama. Vilevile Mhe. Jaji Mwakapeje amewakumbusha kila Mahakama kuendelea na utaratibu wa kutoa elimu kwa Wadau mbalimbali ili kupunguza changamoto za watu kutofuatilia kesi zao na kuchelewa kuisha kwa kesi.
Mhe. Jaji Mwakapeje pamoja na timu yake baada ya kumaliza ukaguzi katika Mahakama ya Mwanzo Muganza walienda Mahakama ya Wilaya Chato. Kwa kuzingatia taratibu walikagua Mahakama hiyo na kusisitiza kuwa uendeshaji wa mashauri ufanyike hatua kwa hatua.
Jaji huyo alimaliza ukaguzi katika Mahakama za Mwanzo Chato Mjini, Bwanga na Buseresere akiwa na timu yake na kuwaomba watumishi wote wafanye kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria. Pia amewataka wajitahidi kuwahudumia wateja kwa uadilifu, uaminifu na weledi.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe.Lukuna amewapongeza watumishi wa Mahakama ya Chato kwa kufanya kazi kwa shirikiano, huku akiwataka waendelee kufuata taratibu na sheria za Mahakama katika kutoa haki kwa wananchi.
Naye Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bi. Kisasila alipongeza jinsi wanavyojituma katika utoaji wa huduma kwa wananchi na aliwakumbusha kuhusu kuwa wepesi na mabadiliko ili kuendana na kasi katika utendajikazi. Vilevile alikazia kuhusu suala la nidhamu katika utumishi wao pamoja na utoaji huduma yenye tija.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Venance Mwakapeje akisaini kitabu cha wageni katika Mahakama ya Mwanzo Buseresere.

(Habari hii imehaririwa na MAGRTETH KINABO,Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni