• Awasisitiza watumishi wa Mahakama kujipanga thabiti kurejesha Imani ya wananchi kwa Mahakama
Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ameanza ziara ya kikazi katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora lengo likiwa ni kukagua shughuli za Mahakama na kukutana na watumishi kuwasikiliza, kutatua changamoto zao, kuwapa motisha sambamba na kuhimiza utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia maadili ya kazi.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake jana tarehe 24 Machi 2025, Mhe. Dkt. Siyani alitembelea katika Wilaya za Igunga, Nzega na Uyui na kufanya mazungumzo na watumishi wa Mahakama hizo.
Akiwa katika ziara hiyo, Jaji Kiongozi aliwataka watumishi kufanya kazi kwa moyo na kujenga utamaduni wa kujituma katika utendaji wao huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kuweka malengo ya kazi na kuyafikia, kuzingatia viwango vya juu vya maadili katika utendaji kazi.
“Ni muhimu kwa watumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa moyo na kujenga utamaduni wa kujituma katika utendaji wao, kila mtumishi anapaswa kuweka malengo ya kazi ya wazi na kuyafikia kwa ufanisi, huku akizingatia viwango vya juu vya maadili katika utendaji wake. Vilevile viongozi wa Mahakama na Kamati za Maadili wanapaswa kusimamia nidhamu kwa ukamilifu na kuchukua hatua stahiki dhidi ya maofisa watakaobainika kukiuka maadili ya kazi. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba Mahakama inabaki kuwa chombo cha kuaminika kinachotoa haki kwa usawa na kwa kuzingatia maadili,” alisema Mhe.Dkt. Siyani.
Kadhalika, Jaji Kiongozi aliwahimiza Viongozi wa Mahakama na Kamati za Maadili kusimamia nidhamu na kuchukua hatua stahiki dhidi ya maofisa watakaobainika kukiuka maadili ya kazi.
Aidha, Jaji Kiongozi pia alikumbusha juu ya umuhimu wa kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama, huku akisisitiza kuwa hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kurejesha imani kwa wananchi ili kuhakikisha utoaji haki unaenda sambamba na wananchi kuiamini Mahakama na mfumo wa mzima wa utoaji haki.
“Ni muhimu sana, tunapaswa kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama. Sisi watumishi wa Mahakama lazima tuchukue hatua thabiti ili kurejesha imani hiyo kwa kuhakikisha kwamba utoaji haki unakwenda sambamba na wananchi kuiamini Mahakama pamoja na mfumo mzima wa utoaji haki, Mahakama inapaswa kuwa ni chombo cha haki kinachozingatia uwazi, usawa na maadili ili wananchi wawe na imani katika mfumo wetu wa haki," alisisitiza Mhe. Dkt. Siyani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kulia) akizungumza na Mhe. William Nchana Hakimu Mkazi baada ya kumaliza kikao na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Uyui katika ziara yake Kanda ya Tabora.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Siyani akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Uyui alipotembelea wakati wa ziara yake jana tarehe 24 Machi, 2025.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akiteta jambo na mwenyeji wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa kwanza kushoto) akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Igunga akiwa ziarani katika Mahakama hiyo jana tarehe 24 Machi, 2025.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa sita kulia) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi kutoka Mahakama Kuu Masjala Kuu na wa Mahakama Kanda ya Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mhe. Sauda Mtondoo aliyesimama akitoa neno wakati wa ziara ya Jaji Kiongozi katika Mahakama ya Wilaya Igunga.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akizungumza na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Zainabu Mango (kulia) wakati wa ziara ya Jaji Kiongozi katika Kanda hiyo aliyoanza jana tarehe 24 Machi, 2025. Aliyesimama nyuma kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Frank Mirindo na aliyesimama nyuma kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Rhoda Ngimilanga.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni