Na Hilari Herman-Mahakama, Lindi
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Elias Kakolaki
amefanya ziara ya siku mbili ya kikazi katika Mahakama zilizopo Mkoa wa Lindi kuanzia
tarehe 24 na 25 Machi, 2025 huku akiwapongeza watumishi kwa kuchapa kazi kwa
bidii.
Ikiwa
ni mara yake ya kwanza kwa Jaji huyo kutembelea Mahakama za ngazi mbalimbali
katika Mkoa huo tangia alipopangiwa majukumu ya kikazi kama Jaji Mfawidhi wa
Kanda ya Mtwara miezi michache iliyopita.
Lengo
la ziara ya Jaji Mfawidhi huyo ni kujitambulisha kwa watumishi kuzungumza na watumishi
wa Mkoa wa Lindi na kujionea mazingira yanayotumika kutekeleze majukumu yao ya
kila siku. Vilevile, kujua hali ya magereza katika mkoa huo na pia kuifahamu
miradi ya ujenzi inayoendelea katika Mkoa huo.
Akizungumza
na watumishi kwa nyakati tofauti tofauti wakati wa ziara hiyo. Mhe. Kakolaki
apotembelea Mahakama za Wilaya ya Kilwa, Ruangwa, Lindi Mjini na Nachingwea
aliwataka watumishi kuwa waadilifu wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa
kuwajibika. “Tukifanikiwa kutekeleza majukumu yetu kwa kugusa nyanja hizo tatu
hakika tutakuwa tumeishi kauli mbiu ya Mahakama ya Tanzania ya Uadilifu, Ueledi
na Uwajibikaji,” alisisitiza.
“Naomba
kila mtumishi atambue kuwa yeye ni Kiongozi katika Kada yake, kwa nafasi yako
unao wajibu na mchango mkubwa katika zoezi zima la utoaji haki kwa wananchi
hivyo basi kila mmoja wetu akatoe huduma ilyobora kwa unyenyekevu, uadilifu,
Lugha nzuri na kuzingatia maadili ya kazi zetu. Hii itasaidia kuboresha taswira
ya Mahakama ya Tanzania na kurejesha imani ya wananchi na jamii kwa Mahakama,”
alisema Jaji Kakolaki.
Aidha,
Mhe. Kakolaki aliwaasa watumishi huo kuachana na matumizi ya karatasi, na hivyo
kujikita zaidi katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA huku akiwasisitiza Mahakimu
kuongeza kasi katika kutumia mifumo ya uratibu wa mashauri ikiwa ni mfumo wa e-CMS
(e-case management system) kwa Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi
na mfumo wa kuratibu mashauri kwa Mahakama za mwanzo (primary court APP) ikiwa
ni sambamba na matumizi ya mifumo mingine yote iliyoanzishwa na Mahakama ya
Tanzania.
Vilevile,
sanjari na kuwataka Mahakimu kutumia mifumo ya kitehama katika usikilizaji wa mashauri,
pia aliwasisitiza Mahakimu hao kuongeza kasi ya usikilizaji wa Mashauri ili
kutozalisha mashauri yenye umri mrefu (backlog).
Aidha,
aliwataka Mahakimu kutoa dhamana kwa Mahabusu ambao wamekidhi vigezo vya
dhamana ili kutimiza haki yao ya kisheria ya kupata uhuru huo. Kwa kufanya
hivyo itapunguza msongamono usiowalazima magerezani na itaongeza nguvu kazi ya
uzalishaji na maendeleo kwa taifa.
Mhe. Kakolaki aliwataka watumishi kujiendeleza
zaidi kielimu kwani itawasaidia
kujiimarisha kimaslahi huku akitoa wito wa kuleana kielemu yaani
(Mentorship) na zoezi hilo la kuleana
kielemu litafunguliwa rasmi kwa kanda hii ya Mtwara hivi karibuni na kusisitiza
kuwa zoezi hilo linagusa kada zote hivyo kila mmoja kwa nafasi yake awe tayari
kumsaidia mwenzake.
Mhe.
Jaji Kakolaki pia alitembelea miradi mitatu ya ujenzi inayoendelea katika Mkoa
huo ikiwa ni pamoja na mradi wa Ujenzi wa kituo kidogo Jumuishi Lindi cha utoaji haki (IJC), Ujenzi
wa Mahakama ya Mwanzo Mitandi iliyopo wilayani Kilwa na Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo
Ndomoni iliyopo wilayani Nachingwea.
Katika
ziara hiyo Mhe. Kakolaki amewataka wakandarasi wanaoendelea na ujenzi wa Miradi
hiyo kuongeza kasi ili majengo hayo yakamilike kwa wakati na kutumika katika
kutoa huduma ya haki kwa wananchi.
Sambamba na hilo, Mhe. Kakolaki aliambatana na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa Mahakama Kanda ya Mtwara na Mkoa wa Lindi wakiwemo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Seraphine Nsana, Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Mhe. Consolata Peter Singano, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Bw. Yusuph Issa Msawanga na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip Godfrey Mbeyela.
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Elias Kakolaki
akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Mhe. Consolata Peter Singano
akiwasilisha taarifa ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi mbele ya Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Elias Kakolaki (hayupo
pichani).
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip Godfrey Mbeyela akifafanua jambo wakati wa ziara ya Mhe.Jaji Mfawidhi (hayupo pichani) kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Bw. Yusuph Issa Msawanga.
Watumishi wa Mahakama mbalimbali kwa nyakati tofauti tofauti Mkoa wa Lindi wakisikiliza kwa makini ujumbe unaowasilishwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Kakolaki (hayupo pichani).
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Elias Kakolaki
akiteta na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa (hawapo pichani).
Watumishi
wa Mahakama mbalimbali kwa nyakati tofauti tofauti Mkoa wa Lindi wakisikiliza
kwa makini ujumbe unaowasilishwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Kakolaki (hayupo pichani).
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Kakolaki akiandika maneno katika ubao wa kumbukizi ulipo katika Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Kakolaki (wa pili kushoto) akikagua miradi ya ujenzi wa kituo jumuishi Lindi.
Ujenzi
wa jengo la Mahakama Kituo Jumuishi Lindi hatua ilipofikia mpaka sasa.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Kakolaki (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali alipokagua gereza
la Wilaya ya Lindi.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Kakolaki akipanda mti katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi.
Watumishi wa Mahakama za Lindi wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Kakolaki wakati wa ziara hiyo
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni