Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama, Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo hivi
karibuni alikabidhi kompyuta mpakato (Laptop) na mashine za kuchapisha nyaraka
kwa Mahakimu wapya saba wa Mahakama za Mwanzo zilizopo Mkoa wa Dodoma kwa ajiri
ya kuwarahisishia utendaji kazi wa kila siku.
Makabidhiano hayo yalifanyika katika ukumbi wa Mahakama uliopo kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe Dkt. Masabo aliwakumbusha Mahakimu hao kuwa matumizi ya teknolojia kwa sasa yamepamba moto mahakamani, hivyo wanapaswa kuitumia vyema wanapotekeleza majukumu yao.
“Mahakama mtandao imeshika kasi tofauti na zamani, nyie mmekuja kipindi ambacho kila kitu kipo kwenye teknolojia. Sote tunapaswa kuitumia teknolojia ipasavyo, hakikisheni mnatumia vizuri Primary Court App katika kusajili mashauri,” alisema.
Jaji Mfawidhi alieleza kuwa anaamini kuna wakati utafika watafanya kila kitu katika mtandao kama ambavyo Mahakama za Wilaya na nyingine zinavyofanya, hivyo Mahakimu hao wanatakiwa kujizoesha kuishi kwenye ulimwengu wa sasa.
Mhe. Dkt. Masabo alitumia fursa hiyo kuwahimiza Mahakimu hao kuzingatia ubora wa maamuzi yao na kuhakikisha wanafanya rejea ya sheria ili waweze kutoa hukumu bora.
Kwa upande wao kwa nyakati tofauti, Mahakimu hao walitoa shukrani kwa uongozi wa Mahakama kwa kuzingatia haja ya kuboresha mazingira ya kazi. Walisema kuwa vifaa hivyo vitawawezesha kufanya kazi zao kwa haraka zaidi na kuleta mapinduzi katika utoaji haki.
Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akikabidhi
vifaa aina ya Laptop na mashine ya kuchapia nyaraka kwa mmoja wa Mahakimu wapya
Mkoa wa Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (katikati) na kushoto kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya
Dodoma, Mhe Silivia Lushasi na kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Dodoma,
Bw.Sumera Manoti wakiwa katika ukumbi wa Mahakama wakati wa hafla fupi ya kugawa
vifaa kwa Mahakimu wapya.
Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo na kushoto
kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe Silivia Lushasi na
kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Bw. Sumera Manoti wakiwa katika
picha ya pamoja na Mahakimu wapya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma
waliohudhuria hafla hiyo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni