Jumatatu, 3 Machi 2025

JAJI MFAWIDHI IRINGA AWAPONGEZA WATUMISHI, WADAU USHIRIKI WA WIKI, SIKU YA SHERIA

Na LUSAKO MWANG’ONDA-Mahakama, Iringa

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Beda Ndunguru, ametoa pongezi kwa Watumishi wa Kanda ya Iringa pamoja Wadau wote kwa kushiriki katika kuadhimimisha Wiki na Siku ya Sheria mkoani Iringa.

Akizungumza katika hafla maalumu iliyopewa jina la “Iringa Law Night Dinner” ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Mount Royal, Jaji Ndunguru alisema kuwa amefurahishwa na ushiriki wa kila mmoja kuanzia Wiki ya Sheria mpaka Siku ya Sheria ambayo iliadhimishwa tarehe 3 Februari, 2025.

“Kwa kweli, ninawashukuru mno kwa majitoleo yenu ya kila kitu. Ndani ya Wiki ya Sheria tulifanya mambo mengi, ikiwa ni pamoja na ushiriki kwenye bonanza la michezo, kutoa elimu katika maeneo mbalimbali na pia kufanya matendo ya huruma na kutembelea vituo vya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu. Nawashukuru sana”. Mhe. Ndunguru alisema.

Hafla hiyo cha chakula cha usiku ilitumika pia kumuaga aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Saidi Kalunde, ambaye kwa sasa amehamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya.

Jaji Mfawidhi alimshukuru Jaji Kalunde kwa utumishi wake uliotukuka akiwa Iringa na kumwomba kwenda kufanya hivyo akiwa Mbeya.

Kwa upande wake, Mhe. Kalunde aliwashukuru Watumishi wote wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kwa ushirikiano waliompa akiwa Iringa na kuwasihi waendelee na ushirikiano huo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Beda Ndunguru akiongea na Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wakati wa hafla hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Angaza Mwipopo akitoa neno kwa watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Saidi Kalunde (ambaye alikuwa anaagwa) akiongea na Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wakati wa hafla hiyo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku akitoa neno kwa Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wa Mahakama wakati wa hafla hiyo.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wa Mahakama wakipata chakula wakati wa hafla hiyo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni