Jumanne, 4 Machi 2025

PROF. OLE GABRIEL ATEMBELEA MAHAKAMA LOLIONDO NGORONGORO MKOANI ARUSHA

  • Akagua Mahakama hizo na kupongeza kwa kutokuwa na mlundikano wa mashauri

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amefanya ziara ya kutembelea Mahakama kadhaa mkoani Arusha lengo likiwa ni kuziona Mahakama hizo na namna zinavyofanya kazi.

Prof. Ole Gabriel alifanya ziara hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo alianza kutemebelea Mahakama ya Mwanzo Loliondo na Mahakama ya Wilaya Ngorongoro ambazo zote zipo katika jengo moja. 

Akiwa mahakamani hapo Mtendaji Mkuu alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa Mahakama hizo pamoja na kukagua mipaka ya maeneo ya Mahakama.

Prof. Ole Gabriel aliwapongeza watumishi kwa kuchapa kazi kwa bidii kufikia kiwango cha kutokuwa na mashauri mlundikano na kusema kuwa, “pamoja na changamoto mlizonazo mnaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na matokeo yanaonekana, tunaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha changamoto mlizonazo zinashughulikiwa, ikiwemo uboreshaji wa mazingira ya kazi na ujenzi wa uzio katika maeneo ya Mahakama.”

Mtendaji Mkuu alisema kuwa, Mahakama imeanzisha Kikosi cha Ujenzi (Building Brigade) ili kurahisisha kushughulikia kazi za ujenzi kama uchimbaji wa visima vya maji, ujenzi wa uzio na ufungaji wa mifumo ya umeme.

Aidha, aliwasifu watumishi ambao ni ajira mpya waliopangwa kufanya kazi Loliondo (Bi. Elizabeth Shirima na Nanjela Elisante), kwa kuendelea kuchapa kazi huku akisema kuwa, watumishi hao ni mfano wa kuigwa kwani Loliondo ni eneo ambalo linachukuliwa kuwa la mbali na lenye mazingira magumu kitu ambacho si kweli, aliongeza kuwa, “ukweli ni kwamba Wilaya ya Ngorongoro ina mazingira mazuri ya kufanyia kazi na zipo fursa mbalimbali za kujiendeleza kijamii na kiuchumi.”

Akiwasilisha taarifa fupi kwa Mtendaji Mkuu, Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro, Mhe. Kohawa Mboya alisema kuwa, Mahakama ya Wilaya na ya Mwanzo Loliondo zilifunga mwaka 2024 bila kuwa na mashauri ya mlundikano na kwamba hali ya usikilizaji wa mashauri ni nzuri licha ya kuwepo kwa changamoto za mtandao.

Naye, Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro, Bw. Benson Fute alizungumzia changamoto ya kutokuwepo kwa uzio katika maeneo ya ahakama, hali ambayo inasababisha mifugo kula miche ya miti inayoendelea kupandwa katika maeneo ya Mahakama. 

Kadhalika, Afisa Tawala huyo alimueleza Mtendaji Mkuu kuwa, Mahakama ya Wilaya Loliondo inakabiliwa na uhaba wa watumishi kwa baadhi ya kada, ikiwemo Walinzi.

Katika ziara yake, Prof. Ole Gabriel alipata fursa pia ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Ketumbeine katika Wilaya ya Longido, ambapo Mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 90 kukamilika, amesifu kasi nzuri ya ujenzi huo kuwa ni mfano wa kuigwa na Wakandarasi wengine.

Kadhalika, Mtendaji Mkuu alitembelea Mahakama ya Mwanzo Enaboishu ambapo alizungumza pia na watumishi pamoja na kukagua mipaka ya eneo la Mahakama hiyo, ambapo aliahidi kuwa uzio kuzuunguka eneo la Mahakama hiyo utajengwa ili kulinda mipaka yake. Amewapongeza watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Enaboishu kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutokuwa na shauri la mlundikano hata moja.

Katika ziara hizo, Mtendaji Mkuu aliambatana na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Loliondo alipotembelea Mahakama hizo hivi karibuni kuona hali halisi ya Mahakama na utendaji kazi wake. Kushoto kwa Mtendaji Mkuu ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya, wa tatu kushoto ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro, Mhe. Kohawa Magreth Mboya.


Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro, Mhe. Kohawa Magreth Mboya akisoma taarifa fupi mbele ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole alipotembelea  Mahakama hiyo hivi karibuni.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na wananchi waliofika katika Mahakama ya Wilaya Ngorongoro na Mahakama ya Mwanzo Loliondo kupata huduma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na watumishi ambao ni ajira mpya, Bi. Elizabeth Shirima (kulia) na Bi. Nanjela Elisante (kushoto) wakati alipotembelea katika Mahakama ya Wilaya Ngorongoro na Mahakama ya Mwanzo Loliondo hivi karibuni.

Jengo la Mahakama ya Mwanzo Loliondo iliyopo katika Wilaya ya Ngorongoro.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Enaboishu alipotembelea mahakamani hapo tarehe hivi karibuni. Kulia kwa Mtendaji Mkuu ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arumeru, Mhe. Itikija Nguvava, wa pili kushoto ni Hakimu wa Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Enaboishu, Mhe. Aisha Athuman na wa kwanza kulia ni Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Arumeru, Bw. Ludovick Macha.

Mtendaji Mkuu akikagua maeneo mbalimbali katika Mahakama ya Mwanzo Enaboishu alipotembelea Mahakama hiyo thivi karibuni.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua maendeleo yaliyofikiwa katika mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Ketumbeine katika Wilaya ya Longido alipotembelea Mradi huo hivi karibuni. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya.

Jengo la Mahakama ya Mwanzo Ketumbeine.

Jengo la Mahakama ya Mwanzo Enaboishu.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Loliondo na kutoa maelekezo alipotembelea Mahakama hivi karibuni. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya.

Nyumba za watumishi wa Mahakama zilizopo 
eneo la Loliondo katika Wilaya ya Ngorongoro.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni