Jumanne, 4 Machi 2025

JAJI RWIZILE AWAPONGEZA WATUMISHI KANDA YA KIGOMA KUSIMAMIA VIZURI RASILIMALI FEDHA

  • Awataka Viongozi kuendelea kuongeza juhudi ya kusimamia eneo la Mirathi katika Mahakama zao

 Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amewapongeza watumishi wa Kanda hiyo kwa kumaliza mwaka bila mashauri ya mlundikano pamoja na usimamizi mzuri wa rasilimali fedha zinazoletwa katika Kanda hiyo kwa ajili ya kuendeshea shughuli za Mahakama.

Mhe. Rwizile alitoa pongezi hizo tarehe 01 Machi, 2025 katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu alipokuwa akifungua kikao cha Kamati ya Uongozi cha tathmini ya shughuli za Mahakama kwa mwaka uliopita na kuweka mikakati wa kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2020/2021-2024/2025 hususani nguzo ya pili ya Upatikanaji na Utoaji Haki kwa wakati. 

“Nimepewa taarifa kuwa takwimu za Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma hatuna kesi za mlundikano na tunakwenda vizuri katika eneo la matumizi ya ofisi Mtandao (e-office) na mifumo mingine ya utendaji wetu, mafanikio haya yamefikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina yetu, hivyo  tuendeleze kudumisha utamaduni huo ili shughuli zetu za kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama wa 2020/2021-2024/2025 ziweze kuwa bora zaidi ya mwaka uliopita,” alisema Jaji Rwizile.

Pamoja na pongezi hizo, Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza mambo kadhaa ikiwemo upandaji miti kwa Mahakama zote zenye nafasi ya kufanya hivyo katika viwanja vya Mahakama, kuongeza weledi wa kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao (virtual Court), kuhakikisha mashauri ya mirathi yanasikilizwa na kumalizika kwa wakati na fedha za mirathi kulipwa kwa wanufaika kwa wakati.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza ambaye ni mlezi wa Mazoezi kwa Kanda ya Kigoma aliwasisitiza wajumbe wa kamati ya uongozi kuhakikisha utamaduni wa kufanya mazoezi kwa watumishi wote unakuwa endelevu kwenye vituo vyao.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akisisitiza jambo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Uongozi kilichofanyika tarehe 01 Machi, 2025 katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akichangia jambo katika kikao cha Kamati ya Uongozi wa Kanda hiyo kilichofanyika tarehe 01 Machi, 2025 katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza akisikiliza kwa makini taarifa ya Kamati ya Uongozi katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika tarehe 01 Machi, 2025 katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kushoto) akikagua ujenzi wa uzio wa Mahakama ya Wilaya Kasulu mara baada ya kumalizika kwa Kikao cha Kamati ya Uongozi kilichofanyika tarehe 01 Machi, 2025 katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao cha Kamati ya Uongozi wa Kanda ya Kigoma. Wa pili ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni