Na DOTTO NKAJA-Mahakama, Geita
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Geita, Mhe. Kevin David Mhina jana tarehe 4 Machi, 2025 alikabidhi Kompyuta Mpakato
(Laptop) kwa Mahakimu Wakazi watano wa Mahakama za Mwanzo walioajiriwa hivi
karibuni na Mahakama ya Tanzania.
Makabidhiano hayo yalikuwa na lengo la kuboresha na
kurahisisha utendaji kazi katika uendeshaji wa mashauri, ikiwa ni pamoja na kwenda
na kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Kanda
hiyo.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita ni kinara wa matumizi
ya TEHAMA katika uendeshaji wa ofisi na usikilizaji wa mashauri.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Mhina aliwaeleza
Mahakimu hao kuwa ili kwenda na kasi ya usikilizaji wa mashauri, ikiwemo utoaji
wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri kwa wakati, ni vyema wakazitumia
kompyuta hizo kwa maslahi mapana ya Taasisi.
Kwa upande wao, Mahakimu hao waliishukuru Mahakama ya
Tanzania kwa kuwapatia vitendea kazi ambavyo vitawawezesha kutekeleza majukumu
yao kwa ufasaha na kwa wakati.
Walisema kuwa kabla ya kukabidhiwa vitendea kazi hivyo
walikuwa wanakumbana na changamoto wakati wa uendeshaji wa mashauri, kwani
walikuwa wakitumia komputa za kuazima na nyingine walizokuwa wanazitumia hazikuwa
na ubora,
Jumla ya kompyuta mpakato tano zilikabiziwa kwa Mahakimu
Wakazi ambao ni Mhe. Eliaman Litahinge Ayoub wa Mahakama ya Mwanzo Ushirombo,
Mhe. Jacob Elinami Shayo wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Rashid Yakweli
Khalfan wa Mahakama ya Mwanzo Bugando, Mhe. Bahati Sultani Omary wa Mahakama ya
Mwanzo Chato Mjini na Mhe. William Greyson Msuya wa Mahakama ya Mwanzo Kharumwa.
Wengine waliohudhuria makabidhiano hayo ni pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kanda ya Geita, Mhe. Fedrick Lukuna, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Geita, Bi. Masalu Kisasila na wengine.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina akikabidhi Kompyuta Mpakato (Laptop) Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Chato Mjini, Mhe. Bahati Sultani Omary.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Geita, Mhe. Kevin David Mhina akizungumza baada ya kukabidhi vitendea kazi kwa
Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo walioajiliwa hivi.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni