Alhamisi, 6 Machi 2025

KAMATI YA KITAIFA YA KUSUKUMA MASHAURI YA JINAI YAKUTANA DODOMA

  • Msajili Mahakama Kuu atoa ujumbe mzito kwa wajumbe

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai leo tarehe 6 Februari, 2025 imefanya kikao kujadili mambo mbalimbali yanayolenga kuharakisha usikilizaji na utoaji haki kwa wakati kwenye mashauri ya jinai.

Kikao hicho ambacho kimefanyika katika moja ya kumbi za mikutano katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma kimeongozwa na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa.

Wajumbe kutoka Taasisi mbalimbali, ikiwemo Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Magereza, Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Chama cha Mawakili Tanganyika na nyingine zinazounda Kamati hiyo wamehudhuria kikako hicho muhimu.

Wakati wa Kikao hicho, wajumbe hao wamejadili mambo mbalimbali, ikiwemo taarifa ya hali ya mashauri ya mlundikano mpaka kufikia mwezi Desemba, 2024, hali ya Mahabusu magerezani na mkakati wa kupunguza mlundikano na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA- kwenye usikilizaji wa rufaa na maombi.

Akizungunza wakati wa kufungua kikao hicho, Mhe. Tengwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, aliwaeleza wajumbe kuwa matumizi ya TEHAMA kwa sasa siyo anasa, bali ni nyenzo muhimu inayohitajika katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

‘Hili ni jambo lisiloepukika. Mahakama ya Tanzania, kwa kutambua hilo, kwa kiwango kikubwa ilijipanga na kuhakikisha kwamba inaachana na tabia za awali na mfumo wa zamani wa kutumia karatasi. Kwa sasa ipo katika mfumo wa kidijitali,’ amesema.

Mhe. Tengwa aliwakumbusha wajumbe wito uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Abdu Kagomba alipokuwa anafungua kikao kama hicho tarehe 9 Februari, 2024 ambapo alisisitiza mambo mbalimbali, ikiwemo uwekezaji mkubwa kwenye mfumo wa TEHAMA.

Mambo mengine yaliyosisitizwa ni kila Taasisi kuajiri watalaam wa TEHAMA, ushirikiano baina ya Taasisi moja na nyingine na kuhakikisha mifumo inasomana na pia Watumishi wa Taasisi hizo kuwa na vifaa stahiki vya TEHAMA ili kuongeza ufanisi katika kazi.

‘Tunaendelea kutoa msisitizo na ushirikiano kwenye dhamira ya dhati ya kutumia TEHAMA. Mahakama ya Tanzania, hususan Mahakama ya Rufani, imekuwa mstari wa mbele katika matumizi ya TEHAMA. Kwa takwimu tulizonazo, asilimia 90 ya vikao vya Mahakama ya Rufani kwa mwezi wa Machi vilifanyika kwa njia ya mtandao. Huko tunakoelekea hakutakuwa na matumizi ya karatasi mahakamani,’ amesema.

Ameelezea matumaini yake kuwa kikao hicho kitatoa mwelekeo na kuwa na maazimio yaliyoshiba yatakayoonesha dhamira ya matumizi ya TEHAMA kwa zaidi ya asilimia 90.


Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa-kushoto-akizungumza wakati anafungua Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai leo tarehe 6 Februari, 2025 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Dodoma. Kulia ni Katibu wa Kamati hiyo, Mhe. Elimo Masawe.


Wajumbe wa Kamati hiyo wakifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa ufunguzi wa kikao hicho.

Sehemu nyingine ya wajumbe wa Kamati-juu na chini-wakiwa katika ukumbi wa mkutano.


Wajumbe wa Sekretariet wakiwa katika kikao hicho

Wajumbe wa Kamati-juu na chini- wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa kikao.


Wajumbe wa Kamati-juu na chini- wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa kikao.

Wajumbe wa Sekretariet wakiwa katika picha ya pamoja.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni