Alhamisi, 6 Machi 2025

KAMATI YA KUSUKUMA MASHAURI MKOA WA IRINGA KUMALIZA MLUNDIKANO MUDA MFUPI UJAO

Na: LUSAKO MWANG’ONDA-Mahakama, Iringa.

Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Jinai Mkoa wa Iringa kimeazimia kwa lugha moja kumaliza mashauri ya mlundikano kwa haraka dani ya muda mfupi ujao.

Maazimio hayo yamefikiwa kwenye kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Japhet Bwire Manyama alisema, azma hiyo itafanikiwa kama wajumbe wote kutoka Taasisi zote za haki jinai zitaamua kuwajibika ipasavyo.

Sisi tuliopo hapa ndiyo wenye maamuzi ya lini tumalize hizi kesi chache za mlundikano. Kama kweli wote mnakerwa na hizi kesi kama ninavyokerwa mimi, hiki kikao kitatoka na majibu ya kuzimaliza haraka iwezekanavyo,alisema Mhe. Manyama.

Kadhalika, Mhe. Manyama aliwakumbusha wajumbe wa kikao kutoa maoni ya namna gani watashirikiana na Mahakama hiyo kuboresha huduma na kurahisisha zoezi la utoaji haki kwa Wananchi pasipo kuchelewesha kesi ili ziishe kwa muda unaotakiwa.

“Mahakama tumejiwekea utaratibu wa kipindi cha kushughulika na haya mashauri, ni aibu kwetu na hata kwenu pia kama Wadau wa haki jinai kuonekana tunashindwa kuzimaliza kesi hizi ndani ya kipindi kilichopangwa,’ alisema.

Aliwaomba waazimie kumaliza mashauri hayo machache yaliyopo na habari ya kesi za mlundikano kwa Mkoa wa Iringa kutojirudia.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu, kikao hicho kilitoka na maazimio ya kuwa kesi zote za mlundikano zilizopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa na Mahakama zote za Wilaya zimalizike tarehe 15 Machi, 2025.

Kadhalika, waliazimia kuwa mashauri yote ya jinai yaliyofunguliwa mwaka 2024 kwenye Mahakama zote kwenye Mkoa wa Iringa yawe yamemalizika ifikapo tarehe 30 Mei, 2025.

Katika kikao hicho, yalijadiliwa masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na msisitizo wa matumizi ya usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (virtual court) ili kwenda na agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania alilolitoa kupitia Waraka Namba 1 wa Mwaka 2025.

Kikao hicho kiliwashirikisha Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi pamoja na wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za haki jinai zilizopo Mkoa wa Iringa kama Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU, Magereza, Polisi, Uhamiaji na kadhalika.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa Mhe. Japhet Bwire Manyama akizungumza wakati wa kikao hicho.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Mhe. Adelina Ngwaya akiwa katika kikao hicho.

Wajumbe wa Kamati ya Kusukuma Mashauri Mkoa wa Iringa wakiwa katika kikao hicho.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni