Jumamosi, 8 Machi 2025

WATUMISHI WANAWAKE WA MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA WATOA MSAADA GEREZA KUU ISANGA DODOMA

  • Ni katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani
  • Maafisa wa Gereza hilo wafurahishwa na zoezi hilo na kutoa rai kwa Watumishi Wanawake kutoka Taasisi nyingine kufanya vivyo hivyo

Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama Kuu Dodoma 

Watumishi wanawake wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jana tarehe 07 Machi, 2025 wametoa msaada wa bidhaa mbalimbali kwa wafungwa Gereza la Isanga lililopo jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake ni tarehe 08 Machi, 2025. 

Akizungumzua wakati wa makabidhiano hayo Afisa Utumishi Mkuu Kitengo cha Rasilimali Watu, Bi. Sharifa Ahmad alisema Mahakama inatambua umuhimu wa kuwatia moyo wanawake walioko gerezani hivyo, wameona umuhimu huo na kuamua kufika kuwaona na kujumuika nao.

“Tumekuja kuwaona na kuzungumza na wanafunzi hawa walioko kwenye mafunzo ya marekebisho hapa gerezani, tumefanya maombi kwa pamoja na tumewapatia bidhaa mbalimbali ikiwa ni ishara ya upendo, kuwajali lakini pia na kuwaunga mkono,” alisema Bi. Sharifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Isanga, Kamishna Msaidizi wa Magereza Zephania Neligwa aliwashukuru Mahakama kwa msaada huo akisisitiza kuwa unawapa wafungwa na mahabusu faraja kubwa na kuwafanya wajione kuwa na wao bado ni sehemu ya jamii.

“Nawashukuru sana kwa msaada huu hakika mnatupa faraja sana tukiona mnakuja kutuona lakini pia tunafurahi sana kuona mnatukumbuka, ni matumaini yangu kuwa taasisi nyingine zitaiga mfano huu wa kutembelea wafungwa na mahabusu wetu,” alisema SCP Neligwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza wa upande wa wafungwa wanawake Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Sifa Aminyike aliwashukuru watumishi hao kwa kuja kuwaona na kuwapa faraja.

Watumishi wanawake walioshiriki katika zoezi hilo walikuwa watumishi wa kada tofauti tofauti kutoka Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

Kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani kitaifa kitafanyika jijini Arusha ambapo Mgeni Rasmi wa shughuli hiyo anatarajiwa kuwa ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.


 Afisa Utumishi Mkuu wa Mahakama ya Tanzania-Makao Makuu, Bi Sharifa Ahmad (wa pili kutoka kulia) akimkabidhi zawadi Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza ambaye pia ni Mkuu wa Gereza kwa upande wa wanawake Isanga, Sifa Aminyike (wa kwanza kulia) wakati walipoenda kutembelea wafungwa hao eneo la Isanga jijini Dodoma jana tarehe 07 Machi, 2025.

Watumishi wanawake kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Askari wa Magereza  walipoenda kutembelea wafungwa na mahabusu waliopo katika Gereza Kuu Isanga-Dodoma tarehe 07 Machi, 2025.

Watumishi wanawake kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Askari Magereza  walipotembelea wafungwa na mahabusu waliopo katika Gereza Kuu Isanga Dodoma jana tarehe 07 Machi, 2025.


Afisa Utumishi Mkuu wa Mahakama Makao Makuu Bi Sharifa Ahmad (wakwaza  kulia) akitoa neno la shukrani kwa mwenyeji wake Mkuu wa Gereza la Isanga, Kamishna Msaidizi wa Magereza Zephania Neligwa mara baada ya kukamilisha ziara hiyo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni