Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma
Menejimenti ya
Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, jana tarehe 26 Machi, 2025 imefanya
kikao cha robo mwaka ili kutathmini utendaji kazi.
Kikao hicho kilichofanyika wilayani Mpwapwa kiliendeshwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo.
Wajumbe wa kikao hicho walipokea taarifa za Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya zilizopo katika Mkoa wa Dodoma na Singida na kuweka mikakati mbalimbali.
Sanjari na hayo, kikao hicho pia kilipokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za kimahakama na kiutawala ambapo maazimio mbalimbali yaliwekwa ili kuhakikisha huduma ya haki kwa Wananchi inawafikia kwa wakati .
Pamoja na mambo mengi yaliyoongelewa katika kikao hicho, Mhe. Dkt. Masabo aliwakumbusha wajumbe kuhusu utoaji haki kwa wakati pamoja na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Jaji Mfawidhi pia aliwataka wajumbe wa kikao hicho kuzingatia kwa umakini maelekezo ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Viongozi wa ngazi za juu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika huduma za utoaji haki.
Kabla ya kufunga kikao hicho, Mhe. Dkt. Masabo aliwaagiza Mahakimu Wafawidhi kufanyia kazi maelekezo yote aliyowapatia na kuhakikisha hakuna mashauri yenye mlundikano na taarifa zihuishwe na kila shauri lina nyaraka muhimu kama ambavyo inatakiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni