Alhamisi, 27 Machi 2025

JAJI MFAWIDHI SHINYANGA AHIMIZA MATUMIZI YA TEHAMA

Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama Simiyu

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali amewahimiza watumishi wa Mahakama ndani ya Kanda hiyo kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwakuwa uwekezaji uliofanywa na Mahakama ya Tanzania katika eneo hilo ni mkubwa sana.

Hayo yamebainishwa jana tarehe 26 Machi, 2025 wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda ya Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.

Jaji Mahimbali amewataka watumishi wa kada zote kuhakikisha wanaijua mifumo yote ya TEHAMA inayotumika ndani ya Mahakama ikiwa ni utekelezaji wa maboresho yanayoendelea kufanyika katika kuwapatia huduma bora wananchi ndani ya Kanda hiyo ambapo alisistiza kwa kusema, “kwa sasa tunayo mifumo mingi ambayo kila mmoja wenu anapaswa kuijua na kuifanyia kazi, mifumo ya kielektroniki kama ya Usimamizi wa Mashauri (e-CMS), Ofisi Mtandao ‘e-office’, ‘e-Wakili’, TanzLII ni baadhi ya mifumo tunayoitumia kila siku, hakikisheni mnaifahamu vema mifumo hiyo.’’ 

Aidha, Mhe. Mahimbali alisema kuwa, Mahakama kwa sasa inaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA na hivi karibuni imeanzisha vioski maalum vilivyokabidhiwa kwa Magereza Dodoma ambavyo vitatumika kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao hivyo wafungwa na mahabusu kutokuwa na haja ya kusafiri kutoka Magereza kwenda Mahakamani. 

“Ni hatua kubwa ya maboresho ya mifumo ya TEHAMA ambayo Mahakama imepiga hivi sasa, zamani ujinga ulitafsirika kama kutokwenda shule, lakini katika karne ya sasa, ukiongelea ujinga ni pamoja na kutokujua matumizi ya TEHAMA, ni dhahiri sisi hatupaswi kuwa miongoni mwa wasiojua matumizi ya mifumo ya TEHAMA, fikisheni ujumbe huu kwa watumishi wote kuwa, kwa sasa kazi kubwa imeelekezwa katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki na tunao wataalam wetu, tuwatumie vijana hawa ili tuweze kuboresha zaidi huduma kwa wananchi,’’ alisisitiza Jaji Mahimbali.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Shinyanga, wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi kwani baadhi ya hoja zilizokuwa zinawasilishwa zimeanza kushughulikiwa, hivyo kwa hoja ambazo bado ziendelee kuwasilishwa Baraza Kuu Taifa ili zishughulikiwe.

Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda ya Shinyanga kilihudhuriwa pia na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Simiyu, Bi. Catherine Nyingi, ikiwa ni maandalizi kuelekea Baraza Kuu Taifa linarotarajiwa kufanyika mapema mwezi Aprili, 2025.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akisisitiza jambo wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo kilichofanyika tarehe 26 Machi, 2025 mkoani Simiyu.

Sehemu ya Wajumbe waliohudhuria Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda ya Shinyanga wakisikiliza hotuba iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali.

Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Kanda, Bw. Robert Nchimbi akifafanua jambo wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Shinyanga kilichofanyika tarehe 26 Machi, 2025 mkoani Simiyu.

Katibu wa TUGHE Mkoa wa Simiyu, Bi. Catherine akifuatilia kwa makini mada zilizowasilishwa wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi Kanda kilichofanyika tarehe 26 Machi, 2025 mkoani Simiyu.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bw. Bakari Mketo akifafanua jambo wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga ambaye pia ni  Mwenyeikiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi -Kanda ya Shinyanga.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni