Jumatano, 12 Machi 2025

SIKU YA KIMATAIFA YA MAJAJI, MAHAKIMU WANAWAKE YAWANUFAISHA WANAFUNZI MBOZI

Na Iman Mzumbwe - Mahakama, Songwe

Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu wanawake  ambayo husherehekewa tarehe 10 Machi kila Mwaka imewanufaisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Nuru iliyopo Wilaya Mbozi  Mkoani Songwe kwa Mahakimu Wanawake  wilayani hapo kuadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu kuhusu makosa ya kimtandao na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.

Akizungumza katika zoezi hilo Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Vwawa mjini Mhe. Martha Malima alitoe elimu kwa wanafunzi hao ya namna unyanyasaji kwa watoto unavyoweza kuleta madhara kubwa katika jamii.

“Nitoe rai kwenu wanafunzi kutojihusisha na vitendo visivyokuwa vya kiungwana na vinavyokiuka maadili mema kama vile kulawitiana, kupiga picha utupu na kushikana sehemu za siri, kufanya hivyo ni kosa la kijinai na adhabu yake ni kifungo au faini au vyote kwa pamoja endapo mtu huyo atathibitika kufanya hivyo,” alisema Mhe. Malima.

Aidha, aliwataka wanafunzi hao kuwa wasiogope kutoa taarifa pindi wanapoona vitendo hivyo kwani kufanya hivyo kutapunguza matendo hayo maovu vitendo hivyo vya unyanyasaji.

Vilevile, ni vema muonapo vitendo hivyo vya ukatili mnaweza kutoa taarifa maeneo kama vile polisi, kwa wazazi, walimu, viongozi wa Serikali za mtaa na maeneo mengine muhimu kulingana na wapi tukio limefanyika.

Naye, Hakimu Mkazi Mahakama ya mwanzo Vwawa mjini, Mhe. Linah Okello alitoa elimu juu ya makosa ya kimtandao jinsi yanavyoweza kuleta athari katika jamii hasa matumizi ya simu za mkononi, umuhimu wa usajili wa laini za simu kupitia Mamlaka ya NIDA, matumizi ya namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine na matumizi mabaya mitandao ya kijamii kama facebook, whatsapp na mitandao mingine ya kijamii yanavyoweza kuchochea unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.

Mhe. Okello aliwaasa wanafunzi hao kuwa, kwa kutumia vibaya mitandao ya kijamii kunaweza kusabisha au kumshawishi mtu akaanza kujihusisha na tabia mbaya za unyanyasaji kama vile kulawiti, kujipiga picha zisizokuwa na maadili katika jamii kama za utupu.

Aidha, Mhe. Okello aliwatahadharisha wanafunzi hao kuwa, matumizi mabaya ya simu yanaweza kusababisha mtu kufunguliwa kesi ya jinai kwa kosa ambalo hajalifanya yeye, mathalani kuazima simu ya mtu mwingine pamoja kwa matumizi binafsi na kusajili laini kwa kutumia namba ya NIDA ya mtu mwingine.

“Niwasihi muendelee kuwa mabalozi kwa watoto wengine, wazazi, walezi na watu wengine katika jamii kwa kufanya hivyo kutasidia kupunguza vitendo na makosa ya bila kujua kama ni matendo ya unyanyaji wa kinjinsia yanayotokea katika jamii,” alisisitiza Mhe. Okello.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo Bw. Festo John Mpepo alisema amefurahishwa na zoezi hilo la utoaji elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo, aliongeza kuwa, ni nafasi ya pekee kwao na elimu hiyo itasidia kuepukana na vitendo ambavyo ni vya unyanyasaji wa kijinsia.

“Nami nitoe rai kwa wanafunzi wangu watumie elimu hii kutusaidia kuielimisha jamii inayotuzunguka juu ya unyanyasaji wa kijinsia na matumizi mabaya ya mitandao yanayoweza kusababisha makosa ya jinai ya kimtandao katika jamii zetu,” alisema Mkuu huyo wa Shule.

Mmoja wa Wanafunzi akiuliza swali kwa watoa elimu (hawapo pichani) wakati wa zoezi la kitoa elimu hiyo shuleni hapo kuhusu makosa ya kimtandao na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.

Mkuu wa shule ya Bw. Festo John Mpepo akitoa shukurani kwa Mahakimu Wanawake wakiwa na baadhi ya Walimu waliokuwa wakiuliza maswali na kupata ufafanuzi zaidi kutoka kwa mahakimu hao

Hakimu Mkazi Mahakama ya mwanzo Vwawa mjini, Mhe. Linah Okello akitoa elimu juu ya makosa ya kimtandao kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nuru mjini Mbozi.

Mahakamu Wanawake wakiwa kwenye picha ya pamoja, Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Vwawa mjini Mhe. Martha Malima (kushoto) Hakimu Mkazi Mahakama ya mwanzo Vwawa mjini, Mhe. Linah Okello (Kulia) ambao ni wawezeshaji wa zoezi la utoaji elimu katika shule ya msingi Nuru Wilaya ya Mbozi

Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Vwawa mjini Mhe. Martha Malima akitoa elimu kwa wanafunzi katika shule ya Msingi Nuru juu ya unyanyaji wa kijinsia.

Waalimu wa Shule ya Msingi Nuru wakiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Manawake waliotoa elimu katika Shule hiyo Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni