Na BAKARI MTAULLAH, Dar es Salaam
Katika kuazimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika tarehe 8
Machi, Watumishi na Viongozi Wanawake wa Mahakama ya Tanzania katika Mkoa Dar-es-Salaam wameungana
na Watanzania wengine kusherekea maadhimisho hayo katika matukio ya aina
tofauti.
Watumishi na Viongozi hao, kwa pamoja walikusanyika katika ukumbi wa PSSSF
kwenye jengo la Golden Jubilee Posta tarehe 7 Machi, 2025 kusherekea Siku hiyo iliyopambwa
kwa Kauli Mbiu isemayo, “Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki, Usawa na
Uwezeshaji.”
Katika sherehe hiyo, washiriki pia walipata elimu jinsi ya utoaji haki
na namna ya kuhakikisha kama kuna usawa katika jinsia zote mbili. Elimu ya uwezeshaji
kiuchumi na kitaaluma pia ilitolewa katika sherehe hiyo.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, alieleza kuwa haki inabadilika kulingana na nyakati, hivyo kila wakati wanatakiwa
kukumbushana haki hizo kwa mtazamo wa wakati husika.
Sherehe hizo zilitamatishwa tarehe 8 Machi, 2025 kwa kutembelea Shule ya
Sekondari Pugu iliyopo Wilaya Ilala, ambapo Watumishi hao, wakiongozwa na Mhe. Dkt.
Opiyo waliwapa faraja Wanafunzi wenye uhitaji maalum na kuwapatia zawadi mbalimbali.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, akitoa neno la ukaribisho kwa
Watumishi hao, alielezea historia fupi ya shule hiyo na pia changamoto
zinazowakabili watoto hao kwa sasa. Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Wazazi
kutowaficha watoto wenye mahitaji maalum kwa kuhisi kuwa wana mkosi.
‘Watoto hawa wana uwezo mkubwa sana kielimu kiasi cha kwamba wana muda
mrefu hawajawahi kupata Daraja la Nne,’ alisema.
Mkuu wa Msafara aliwapongea Walimu hao kwa hatua hiyo na kuwasihi wawe
na moyo huo wa kuwalea vijana hao, kwa kuwa nao licha ya kuwa ni Walimu lakini
pia ni Wazazi.
“Sisi katika kusherekea Siku ya Wanawake Duniani hatuna ubaguzi,
hatuangalii Wanawake tu, tunaangalia pia wenye uhitaji kuliko jinsia au jinsi,’
alisema.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni