Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kanda ya Kigoma ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo, ametoa rai kwa wadau wa Mahakama katika Kanda hiyo kushirikiana kufanya kaguzi katika magereza na kutatua changamoto zinazoibuliwa kwenye kaguzi hizo na kuzitatua kwa pamoja.
Mhe. Tarimo alitoa rai hiyo tarehe 04 Aprili, 2025 alipokuwa akiongoza kikao cha wadau wa kusukuma mashauri ya jinai Mahakama Kanda ya Kigoma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Jengo la Mahakama Kuu Kigoma hiyo tarehe 04, Aprili 2025.
Kikao hicho kilikuwa cha kutathmini mwenendo wa utoaji haki katika mashauri ya jinai na kubaini changamoto na kuziwekea mikakati ya kuzitatua kwa haraka ili kuendana na kasi ya utoaji haki kwa wakati kwa kuzingatia mchango wa kila mdau kutimiza wajibu wake katika mnyororo wa haki jinai.
Mhe. Tarimo aliwasisitiza kuwa, Mahakama ipo wazi kutatua na kushirikiana na mdau yeyote mwenye nia ya kushirikiana na kuboresha utendaji kazi wa Mahakama hasa katika kuwahisha usikilizwaji wa mashauri mahakamani na kuboresha vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwakuwa Mahakama imejipambanua katika matumizi ya Teknolojia.
“Hii ni kwa sababu TEHAMA, imekuja kurahisisha na kupunguza gharama za wananchi katika kuitafuta haki katika Mahakama zetu hapa Kigoma,” alisema Mfawidhi huyo.
Hivyo, Mhe. Tarimo aliwataka wadau hao kushirikiana na Mahakama kutekeleza maelekezo ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania ya kusikiliza mashauri ya Maombi na rufaa zote kwa Mahakama Kuu, kwa njia ya Mahakama mtandao (Virtual Court) ili kupunguza gharama na muda kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kigoma, Bw. Waziri Magumbo alisema kuwa, ofisi hiyo inaendelea kujiwekea viwango vya uendeshaji wa mashauri mahakamani kwa miezi sita tu, ndio uwe umri mrefu wa shauri linalosimamiwa na ofisi hiyo mahakamani katika Kanda hiyo.
Bw. Magumbo alibainisha kuwa, kutekeleza mkakati huo ni juhudi kubwa za ofisi hiyo kuisaidia Mahakama kumaliza mashauri kwa wakati na kutekeleza mkakati wa Mahakama utoaji haki kwa wakati.
Alisema kuwa, ofisi yake haitakuwa kikwazo cha kukwamisha shughuli za Mahakama katika usikilizwaji wa Mashauri ya jinai yaliyopo katika Mahakama Kanda ya Kigoma.
Kwa upande wake Mjumbe mwalikwa wa kikao hicho kutoka Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) ambaye ni Afisa Hifadhi Mshirika, Bi. Rehema Msami alisema kuwa, kwa niaba ya shirika hilo wataisaidia Mahakama ya Mwanzo iliyopo katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu ili Hakimu anayehudumu katika Mahakama hiyo aweze kutumia vifaa vya kisasa kulingana na mifumo ya Mahakama ya Tanzania ili kuwahisha haki kwa wakimbizi waishio katika kambi hiyo.
Bi. Rehema alisema kuwa, shirika hilo litaendelea kushirikiana na Mahakama katika kuboresha vitendea kazi vya kitehama katika Mahakama za Kanda ya Kigoma.
Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo akisisitiza jambo wakati wa Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Jinai Mahakama Kanda ya Kigoma kilichofanyika tarehe 04 Aprili, 2025 katika ukumbi uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma.
Sehemu ya wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Jinai Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kanda ya Kigoma.
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kigoma, Bw. Waziri Magumbo akifafanua jambo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa maazimio wakati wa kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Jinai Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kilichofanyika tarehe 04 Aprili, 2025 katika ukumbi uliopo Mahakama Kuu Kigoma.
Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma, ACP Mwesa Nyamwihwagya akitoa taarifa ya Magereza kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025 wakati wa Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Jinai kilichofanyika tarehe 04 Aprili, 2025 katika ukumbi uliopo Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Mjumbe mwalikwa ambaye ni Afisa Hifadhi Mshirika kutoka Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR), Bi. Rehema Msami akizungumza jambo katika Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Jinai Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kilichofanyika tarehe 04 Aprili, 2025.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni