Jumamosi, 5 Aprili 2025

KWA TAKRIBANI MIAKA 100 MAHAKAMA YA TANZANIA YAANDIKA HISTORIA YA KIPEKEE

·       Wananchi na wadau wafurahishwa na miundombinu ya kisasa ya Mahakama

Na Salum Tawani na Arapha Rusheke- Mahakama, Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa, kwa mara ya kwanza Mahakama ya Tanzania kuwa na Ofisi yake ya Makao Makuu ya Mahakama italeta tija katika kutekeleza Majukumu yake kwa ufasaha.

Amezungumza hayo katika uzinduzi wa Makao Makuu ya Mahakama uliofanyika katika eneo la Tambuka Reli lililopo jijini Dodoma leo tarehe 05 Aprili, 2025.

“Kwa uzinduzi wa majengo haya na mambo mengine ambayo yameonekana kwa Watanzania siyo tu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenda haki bali sisi Watanzania wote tumeona haki ambayo ameutendea Mhimili wa Mahakama, Sekta ya Sheria na Sekta ya haki,” alisema Mhe. Dkt. Ndumbaro.

Aidha, Waziri huyo amesema kuwa, amefurahishwa na ujenzi huo ambao umewashirikisha wazawa na mchango wa maudhui ya asili (Local Content) wa wazawa kwenye kazi hiyo ni asilimia kubwa, na asilimia 95 ya wataalam kwa maana  wahandisi ni Watanzania na Mshauri elekezi ni kampuni ya Kitanzania, hiyo ni hatua muhimu ya kuwajengea uwezo wataalam wa ndani pamoja na makampuni ya wazawa, niwaombe Wizara na Taasisi zingine za Kiserikali zizingatie umuhimu wa kuwashirikisha wazawa katika miradi mikubwa kama ilivyofanya Mahakama.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema imekuwa ni historia kubwa kwa  Dodoma ilikuwa na  Mhimili miwili na leo Mhimili wa tatu umekamilika na  kuwa Makao Makuu  ya Nchi, hiyo ni historia ya pekee ambayo itakuandika Mhe. Rais katika vitabu vyote vya historia ya nchi ya Tanzania.

“Mhe Rais dhamira yako ya kutaka haki tunaiona jinsi wakati wote umetamani Watanzania watendewe haki lakini jinsi ambavyo umetamani ardhi ya Tanzania iandike haki kwa kila Mtanzania anayekanyaga katika nchi hii,” alisema Mhe. Rosemary...

Mambo haya Mhe. Rais  tumeyaona ukiyasema kwa maneno yako na tumeyasikia  lakini zaidi  tumeona kwa vitendo ambavyo umekuwa ukifanya  vya kutenda haki, mfano mdogo tu  ulipoanzisha Mama Samia Msaada wa Kisheria (Mama Samia Legal Aid) kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ulitaka hata watu wa chini wapate haki yao katika nchi yetu ya Tanzania,” alisema Mhe. Rosemary

Mhe. Senyamule amesema, jambo linaloonekana la kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utayari wa kujenga majengo kubwa ya kisasa ya Mahakama inaonyesha dhamira yako ya dhati ya kutaka haki kwa kila Mtanzania.

Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kutengeneza historia ya Mapinduzi makubwa katika Mhimili wa Mahakama ambao Dunia inashuhudia majengo lakini amefanya na mambo mengine mengi ameyafanya katika kipindi chake.

Ni wazi kuwa, majengo yanayozinduliwa yatafanya watumiaji wafanye kazi kwa furaha, amani na utulivu na kupelekea kuwatendea haki Watanzania wote ambao watapata huduma katika eneo hilo.

Vilevile, viongozi wa dini kwa nyakati tofauti wametoa pongezi kwa uongozi wa Mahakama kwa hatua hiyo ya kuwa na majengo yao katika Mkoa wa Dodoma kwani imekuwa ni faraja na jambo la kihistoria katika Nchi kushuhudia Majengo mazuri nay a kisasa yakizinduliwa.

Wananchi nao hawakuwa nyuma wameipongeza sana Mahakama ya Tanzania kwa kuboresha miundombinu ya Mahakama na kushukuru kwa kupata majengo ya kihistoria katika Mkoa wa Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas D. Ndumbaro (Mb) akiongea neno la shukrani wakati wa ufunguzi wa Majengo ya Mahakama leo tarehe 05 Aprili, 2025 jijini Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Sitaki Senyamule akitoa sifa kemkem wakati akizungumza kwenye hafla ya ya ufunguzi wa majengo ya Mahakama .


Ufunguo wa Dhahabu ukikabidhiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama. 
Sehemu ya Wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama wakifuatilia kwa umakini uzinduzi huo uliofanyika Tambukareli eneo iliyopo mahakama hiyo.





Sehemu  ya Wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama wakifuatilia kwa umakini uzinduzi huo uliofanyika Tambukareli eneo iliyopo mahakama hiyo.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha -Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni