·
Rais
Samia akiri kuwa jengo hilo lina hadhi na sifa ya kuwa Makao Makuu ya Mahakama
·
Aipa
kongole Mahakama kwakuwa na Mifumo ya TEHAMA inayosomana na kuzitaka Taasisi nyingine
za Serikali kuiga
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan leo tarehe 05 Aprili, 2025 ameweka historia kwa Mhimili wa
Mahakama kwa kuzindua rasmi Jengo la kwanza la Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania na kukiri kuwa jengo hilo la kisasa na la Kimataifa lina kila sifa na
hadhi ya kuwa Makao Makuu ya Mhimili huo.
Uzinduzi wa jengo hilo ni hatua kubwa kwa historia ya
Mahakama nchini kufuatia ukweli kwamba, Mhimili huo haukuwahi kuwa na jengo la
makao makuu kwa kipindi cha miaka 104 tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza wakati akitoa hotuba yake kwenye hafla ya
uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa
Jengo la Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na Nyumba 48 za Makazi ya
Majaji, Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa, hatua ya upatikanaji wa jengo hilo ni moja
ya maboresho makubwa yaliyofanyika ndani ya Mhimili wa Mahakama lengo likiwa ni
kuboresha huduma ya upatikanaji haki.
“Leo tumeandika historia nyingine kubwa zaidi kwa
upande wa Mahakama na Nchi, ni zaidi ya ile ya awali ya uzinduzi wa majengo ya
Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) sita. Nimelikagua jengo hili kwenye baadhi
ya Ofisi zikiwemo Vyumba vya Magereza, Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa
mbalimbali za Mahakama, Ofisi za Mawakili Watoto na nikiri kuwa lina kila sifa
la kuwa Makao Makuu ya Mahakama,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia hakusita kuipongeza Mahakama ya
Tanzania chini ya Uongozi wa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kuendelea kuwa mfano
mzuri wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ambapo ameonesha
kufurahishwa na Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za
Mahakama (Judiciary Visual Situation Room).
“Nimeona Chumba maalum cha Mifumo ya utoaji taarifa
mbalimbali (Judiciary Situation Room) ambayo nimeambiwa ni ya pili kwa ukubwa
duniani, kwakweli nimeshangazwa na yaliyomo ndani, tunayoyashuhudia leo ni
matokeo ya tuliyashuhudia kwenye nchi za wenzetu,” amesema Mhe. Samia.
Ameongeza kuwa, Serikali inachukua suala la utoaji wa
haki kwa uzito wa pekee na kwamba mpaka sasa jumla ya miradi 144 ya ujenzi na
ukarabati wa majengo ya ngazi mbalimbali za Mahakama unaendelea na kuahidi kuwa,
miradi itakamilika kwa wakati.
Rais Samia, amebainisha kuwa kazi iliyofanywa na Mahakama
ni zaidi ya kile kilichoahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na
Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa, “Serikali
itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wake kadri uwezo wa kibajeti
utakavyoruhusu.”
Kwa upande mwingine, amewakumbusha watumishi wa
Mahakama kuimarisha utoaji wa huduma ya haki kwa wananchi na kugusia juu ya umuhimu
wa Mahakama za Mwanzo kutofungwa na masharti ya kiufundi yanayozuia haki
kutendeka kwa wakati.
Katika hotuba yake, Rais Samia amewasisitiza pia watumishi
wa Mahakama kuhusu utunzaji wa miundombinu ya majengo ya Mahakama ambapo
amekazia kwa kusema kwamba, “Jengo hili la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania
na mengine niliyoyazindua nikipita hata baada ya miaka mitatu yawe hivihivi
kwakuwa gharama za ukarabati ni kubwa.”
Ameikumbusha pia Mahakama kufanya maboresho ambayo pia
yanazingatia Mahakama maalum mfano Mahakama ya Ardhi, Mahakama ya Masuala ya
Familia na kadhalika.
Miradi mitatu iliyozinduliwa leo imegharimu kiasi ya fedha za kitanzania bilioni 185.4. Kupatikana kwa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama kunafanya Mihimili yote mitatu ya Dola ikiwemo Serikali na Bunge kuwepo Makao Makuu ya Nchi jijini Dodoma.
Nyumba 48 za Makazi ya Majaji ambazo zimezinduliwa leo pia na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Sehemu ya Viongozi mbalimbali wa Serikali, Watumishi wa Mahakama ya Tanzania pamoja na wageni waalikwa wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Nyumba za Makazi ya Majaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni