Na INNOCENT KANSHA - Mahakama
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani leo
tarehe 23 Aprili, 2025 amefungua Kongamano la mafunzo ya Usalama Mahala pa Kazi
kati ya Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, Taasisi ya Wakala wa
Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) pamoja taasisi za kiserikali ambazo ni wadau
wa Mahakama Kazi.
Kongamano la mafunzo
hayo yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa jengo la OSHA
limebeba Kauli mbiu maalum kwa ajili ya kutafakari na kubadilishana uzoefu juu
ya “Nafasi
ya Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) Mahali pa Kazi (Mapinduzi na
Fursa)”
“Kwa kuwa nyinyi ni wadau wa utoaji haki na huduma katika sekta
mbalimbali, mafunzo haya ni muhimu sana kwenu. Matumizi ya akili unde yamedhihirika kuleta mafaniko na ufanisi katika sekta
mbalimbali duniani. Tanzania sio kisiwa na hivyo hatuwezi kubaki nyuma. Ni
lazima nchi yetu iendane na mabadiliko chanya ya kiteknolojia na utendaji
yanayotokea kote ulimwenguni. Mafunzo haya yanatoa fursa ya kupiga hatua muhimu
katika safari ya uboreshaji wa mifumo na utendaji kazi wetu,”. amesisitiza Jaji
Kiongozi Mhe. Dkt. Siyani.
Jaji Siyani amendelea kwa kusema, akili unde ni matokeo ya kuongezeka kwa utafiti na kukua kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kiasi cha kuwezesha kutengenezwa kwa mifumo yenye utambuzi wa mambo mfano wa binadamu. Viwango vya usahihi vinavyozidi kuongezeka kadri ya mifumo hiyo inavyotumiwa na muda mfupi ambao mifumo hiyo inatumia kutekeleza kazi mbalimbali, vinaongeza hamasa na kuonyesha umuhimu wa matumizi yake.
Mhe.
Dkt. Siyani ameongeza kuwa, matumizi ya akili unde yanazaa fursa na changamoto
mbalimbali kupitia mafunzo washiriki watapata nafasi ya kupitia faida na hasara
za matumizi ya akili unde. Faida za matumizi ya akili unde ni nyingi na kama
nilivyotangulia kusema ni pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kurahisha tatifi mbalimbali,
kutafsiri lugha, kupunguza makosa ya kibinadamu, pamoja na kuokoa muda na
gharama.
“Aidha,
akili unde inaweza kuwapa wafanyakazi muda zaidi wa kufikiria mambo yenye tija
kubwa zaidi kwa taasisi na kutunza kumbukumbu muhimu kazini, mambo yanayoweza kukuza ugunduzi na
ushindani,” amesema Mhe. Dkt. Siyani.
Aidha, Jaji
Kiongozi ameongeza kuwa, akili unde haikuja na faida pekee bali pia, inazo
changamoto zake. Moja ya changamoto hizo ni hofu ya watu kudhani kuwa
watapoteza kazi zao ikiwa akili unde itaachwa kuendelea kukua na kufanya kazi ambazo
kimsingi zinafanywa na binadamu. Hofu nyingine ni kupotea kwa usiri na
uwezekano wa taarifa muhimu
kudukuliwa.
“Ni muhimu kujua kuwa katika dunia yetu ya
sasa matumizi ya akili unde hayakwepeki. Iko haja ya kujadili na kuhakikisha
kwamba kila mmoja anajiongezea thamani kama mfanyakazi ili kufikia viwango na
kufanya kazi ambazo haziwezi kufanywa na akili unde, lakini pia kuhakikisha
kuwa mifumo yetu imewekewa ulinzi wa kutosha kudhibiti matumizi mabaya ya akili
unde kwa ajili ya udukuzi wa taarifa,” amesema Jaji Siyani.
Vilevile, Mhe.
Dkt. Siyani amesema kwamba, uzoefu watakaoupata washiriki wa mafunzo hayo,
utawapa jukumu la kuhakikisha kuwa matumizi ya akili unde yanawasaidia
kuboresha utendaji kazi kama mtu mmoja mmoja na ufanisi wa taasisi. Ni matumaini
ya Mahakama na taasisi zingine zinazoshiriki mafunzo ya akili unde yatawapa pia
ujuzi wa kukabiliana na changamoto zitokanazo na maendeleo ya teknolojia katika utendaji kazi.
Aidha, Jaji
Kiongozi akatoa rai kwa washiriki wa mafunzo kutumia nafasi ya mafunzo hayo
ipasavyo kubadilishana uzoefu, kujielimisha, na kutoa maoni ya namna ya
kuboresha utendaji wa kazi, lakini pia sheria na sera zinazosimamia matumizi ya
akili unde pamoja na usalama na afya kwa watumishi kwa ajili ya kulinda maslahi
ya wafanyakazi.
Akihitimisha hotuba yake ya
ufunguzi wa mafunzo Mhe. Dkt. Siyani ameushukuru
uongozi wa OSHA kwa kutambua uhitaji wa mafunzo hayo kwa watumishi wa umma na kukubali kuwezesha kufanyika kwake kwa
mara ya pili jijini Dodoma.
“Ni rai yangu kuwa
ushirikiano huu baina ya OSHA kama mdau wa Mahakama uendelezwe ili kuwapa
watumishi wa umma wakiwemo wale wa Mahakama fursa ya kupata elimu na
kubadilishana uzoefu kupitia mijadala mbalimbali itakayoongeza tija kazini...
Aliwashukuru wafanyakazi wa
Mahakama na wa Taasisi nyingine za umma kwa kutenga muda na kuja kushiriki
mafunzo haya muhimu. Ni matarajio yangu kuwa baada ya mafunzo haya, washiriki
watarejea katika maeneo yao ya kazi wakiwa na maarifa mapya yatakayowasaidia
kuongeza tija, kuboresha utoaji wa haki na huduma bora kwa wananchi,” ameongeza
Jaji Siyani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akifungua Kongamano la mafunzo ya Usalama Mahala pa Kazi kati ya Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, Taasisi ya Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) pamoja taasisi za kiserikali ambazo ni wadau wa Mahakama Kazi leo tarehe 23 Aprili, 2025 jijini Dodoma katika Ukumbi wa jengo la OSHA.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akifungua Kongamano la mafunzo ya Usalama Mahala pa Kazi kati ya Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, Taasisi ya Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) pamoja taasisi za kiserikali ambazo ni wadau wa Mahakama Kazi leo tarehe 23 Aprili, 2025 jijini Dodoma katika Ukumbi wa jengo la OSHA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni