Alhamisi, 24 Aprili 2025

JAJI DKT. MLYAMBINA AHAIDI MAHAKAMA YA KAZI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA OSHA

Na ARAPHA RUSHEKE- Mahakama, Dodoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina jana tarehe 23 Aprili, 2025 ameongoza Kikao kazi cha watumishi wa Mahakama ya Tanzania kutoka sehemu mbalimbali wakiwemo waheshimiwa Majaji Wafawidhi, Majaji, Naibu wasajili, Mahakimu, Wasaidizi wa sheria wa Majaji, watendaji wa Mahakama na viongozi mbalimbali wataasisi za kiserikali zinazofanya kazi katika mnyororo wa Mahakama kazi.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) uliopo tambukareli jijini Dodoma

Akizungumza wakati wa neno la utangulizi wa Kikao hicho, Mhe. Dkt. Mlyambina alieleza kuwa Mafunzo haya ni sehemu ya mwendelezo wa ushirikiano mwema kati ya Mahakama na OSHA ushirikiano ulioanza kuimarika tangu kufanyika kwa mafunzo ya awali yaliyohusisha Watumishi wenye ulemavu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na Kanda tofauti za Mahakama.

“Awamu hii ya pili, tunajivunia kuwahusisha viongozi wa Mahakama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Ofisi ya kamishina wa Kazi, CMA pamoja na viongozi kutoka OSHA, jambo ambalo linadhihirisha dhamira ya dhati ya Muhimili wa Mahakama na Serikali katika kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wananchi. Ushirikiano huu ni utekelezaji wa Nguzo ya Tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya mwaka 2020/2021– 2024/2025, inayolenga kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama pamoja na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama,” Jaji Mfawidhi huyo alisema.

Aliendelea kubainisha kuwa katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi, maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yameleta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo Sekta ya Haki-Kazi. Matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) ni nyenzo muhimu ya kuongeza tija, kupunguza gharama za uendeshaji, na kuharakisha utoaji wa maamuzi kwa wakati. Ni kwa msingi huo, kauli mbiu ya mafunzo haya inasema: "Nafasi ya Akili Unde (Artificial Intelligence –AI) Mahali pa Kazi (Mapinduzi na Fursa)." Kauli mbiu hii si tu inasisitiza umuhimu wa teknolojia, bali pia inatufungua macho kuhusu nafasi ya AI katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kuhakikisha usalama wa watumishi, na kupunguza hatari kazini.

Katika salamu zake za ukaribisho Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kundeleza ushirikiano mzuri na muhimili huo katika kutambua umuhimu wa usalama mahala pakazi kupelekea kukubali watumishi kushiriki mafunzo hayo ambayo yatawasaidi na kuwajengea uelewa washiriki katika masuala ya usalama na afya waweze kutekeleza maşukumu yao yake kila siku kwa kuzingatia kanuni bora na kujilinda dhidi ya viatarishi vya magonjwa na ajali mahala pa kazi.

Naye, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Hadija Mwenda aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kujifunza vitu vingi na kwaweredi mkubwa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina akitoa neno la ukaribisho wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usalama mahala pa kazi kwa watumishi wa mahakama na taasisi za mnyororo wa Mahakama Kazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa neno wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Hadija Mwenda aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kuwashukuru washiriki hao
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Dkt.Mustapher Mohamed Siyani ikiwa katika picha ya pamoja na wadau kutoka OSHA waliohudhuria mafunzo hayo.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha- Mahakama)







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni