Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa wito kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani
Tanzania kubuni mbinu mpya zitakazosaidia kukabiliana na ongezeko la mashauri
kutoka Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya.
Mhe. Prof. Juma ametoa
wito huo leo tarehe 24 Aprili, 2025 alipokuwa anafungua Mkutano wa Mwaka 2024 unaofanyika
kwa siku mbili kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam, kujadili masuala mbalimbali katika Mahakama ya Rufani na Mahakama ya
Tanzania kwa ujumla.
‘Hiki ni kikao cha
kupanga mikakati juu wajibu wetu katika kukabiliana na ongezeko la mashauri
baada ya kukamilika ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki tisa na Mahakama
za Mahakimu 60 zinazoendelea kujengwa…
‘…Katika kikao hiki
tutakaribisha majadilino yatakayotusaidia kuendelea kubaini maeneo muhimu
ambayo bado yanaleta changamoto katika utekelezaji wa majukumu yetu na kutafuta
mbinu za kuondokana na changamoto hizo.’ Jaji Mkuu amesema.
Amebainisha kuwa takwimu
zinaonyesha idadi ya mashauri yanayofunguliwa Mahakama ya Rufani kwa mwaka
imeendelea kuongezeka na kwamba Mkuu wa Idara ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano-TEHAMA- amefanya makisio ya mzigo ambao Majaji 39 wataubeba kuanzia
mwaka 2026 hadi 2030.
Mhe. Prof. Juma
amebainisha kuwa kila Jaji wa Mahakama ya Rufani amekadiriwa uwezo wa kushughulikia
rufaa 99 kwa mwaka, hivyo uwezo wa Majaji wa Mahakama ya Rufani 39 ni kushughulikia
rufaa 3,861 kwa mwaka.
Amesema kuwa makisio ya ongezeko
la rufani kuanzia 2026 hadi 2030 yatakuwa mashauri 10,434 kwa mwaka 2026,
mashauri 11,248 mwaka 2027, mwaka 2028 mashauri 12,061, mwaka 2029 mashauri 12,875
na mwaka 2030 ni mashauri 13,690, huku kila mwaka Majaji hao wakiwa na wastani
wa kushughulikia mashauri 3,861.
‘Hatuwezi kukabiliana na
wingi na ongezeko la mashauri yanayotiririka kupitia ngazi na vituo mbalimbali
hadi kuishia katika Mahakama ya Rufani kwa kutegemea tu mpangilio wa kisheria,
kanuni na idadi ya Majaji wa Rufani na Majopo yaliyopo,’ Jaji Mkuu amesema.
Amebainisha kuwa Mkutano
huo wa Majaji wa Rufani, uwe mwanzo wa kujiwekea mikakati ya kuziangalia
sheria, kanuni na kuzichakata upya taratibu za Mahakama ya Rufani na zile za
Mahakama za ngazi za chini ili kumudu ongezeko kubwa la mashauri.
Akizungumzia mlundikano
wa mashauri, Jaji Mkuu amebainisha kuwa mwaka 2024, Mahakama ya Rufani ilikuwa
na mashauri ya mlundikano 1,273, sawa na asilimia 21 ya mashauri yake na
kuchangia asilimia 74 ya mlundikano wa mashauri ulioko mahakamani katika ngazi
zote, huku ngazi zingine za Mahakama zikiweza kudhibiti changamoto hiyo.
Ameeleza pia kuwa kati ya
Januari na Desemba 2024, wakati Mahakama ya Rufani ilikuwa na asilimia 21 ya
mashauri ya mlundikano, Mahakama Kuu haikuwa na tatizo hilo kwani mwaka 2024,
mlundikano ulikuwa ni asilimia 2 tu, Mahakama za Hakimu Mkazi ulikuwa asilimia
6 pekee na Mahakama za Wilaya zilikuwa asilimia 1 na Mahakama za Mwanzo
hazikuwa na mlundikano mwaka 2024.
‘Kwa ulinganifu wa ngazi
zote za Mahakama, hali yetu Mahakama ya Rufani sio nzuri katika mlundikano,
tunachangia asilimia 74 ya mzigo wa mlundikano katika ngazi zote za Mahakama ya
Tanzania,’ Mhe. Prof. Juma amesema.
Jaji Mkuu amesisitiza
matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma za kimahakama kwani ni njia bora ya
kupambana na changamoto hiyo na amewapongeza Majaji wote kwa kuanza utekelezaji
wa jambo hilo.
‘Tunaomba tusirudi nyumba,
tuendelee kusikiliza mashauri yote kwa njia ya mfumo na tuendelea kubaini
changamoto na kuziwasilisha kwa wajenzi wa mfumo ili tuendelee kuboresha zaidi
mfumo na kurahisisha utendaji kazi,’amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwapongeza
Majaji na Watumishi wote wa Mahakama ya Rufani kwa kuendelea na jitihada za
kuamua mashauri kwa mafanikio makubwa, licha ya changamoto mbalimbali
mnazokabiliana nazo.
Wakati wa Mkutano huo,
wajumbe watapokea na kujadili taarifa mbalimbali zinazohusu mashauri katika
Mahakama ya Rufani pamoja na masuala mbalimbali ya kiutumishi, ikiwa ni pamoja
na ikama, bajeti, stahiki za Majaji, mabadiliko ya sheria kwenye stahiki za Majaji
pamoja na mafunzo kwa watumishi wa Mahakama ya Rufani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni