Jumanne, 22 Aprili 2025

JAJI MFAWIDHI AAGIZA MRADI WA IJC KUKAMILIKA KWA HARAKA


NA. ALLY RAMADHANI – Mahakama, Katavi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Fedrick Kapela Manyanda, ameagiza kuitaka Mkandarasi wa Kampuni ya M/s AZHAR Construction Co. Ltd kukamilisha ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Katavi kinachoendelea kujengwa Mkoani Katavi kwa wakati na kuzingatia viwango na ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa mkataba.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Fedrick Kapela Manyanda, ametoa maelekezo hayo mahsusi jana tarehe 21 April, 2025 kwa timu ya usimamizi wa mradi huo wa ujenzi ilikuwa ikiongozwa na Mhe. Naibu Msajili wa Mahakama Mussa Hamza pamoja na Mhandisi Fabian Kwangilwa kuendelea kusimamia kazi na kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika katika muda uliopangwa.

Aidha, Mhe. Jaji Mfawidhi alipata wasaa wa kukagua shughuli zinazoendelea katika mradi wa ujenzi wa Kituo hicho, na kujionea maendeleo yake, likiwemo jengo dogo la mgahawa litakalomilikiwa na Mahakama.  Eneo lingine lililokaguliwa ni uzio wa jengo ambao tayari umeanza kujengwa kwa kasi.

Pia Mhe. Manyanda Sumbawanga aliongeza “nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa jengo la IJC KATAVI na nipende kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua iliyochukua ili kusaidia kukamilika kwa mradi huu.”

Moja ya nguzo katika Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ni Utoaji Haki kwa Wakati. Hivyo Mahakama inatekeleza mpango huo kwa kuboresha mazingira ya utoaji haki na kusogeza huduma za utoaji haki kwa wananchi kwa kujenga miundombinu bora na wezeshi itakayochangia ufanisi mzuri wa utekelezaji wa nguzo hii. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Fedrick Kapela Manyanda (wa pili kushoto), alipotembelea mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Katavi) kinachoendelea kujengwa mkoani Katavi.

P
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Fedrick Kapela Manyanda (wa pili kushoto), pamoja na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Bw.  Epaphras   Tenganamba (wa pili kutoka kulia), Naibu Msajili wa Mahakama (wa kwanza kushoto) Mhe. Mussa Hamza, akiwemo  Mhandisi Fabian Kwagila (wa kwanza kulia) walipotembelea mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki(IJC), Katavi kinachoendelea kujengwa mkoani Katavi.

(Habari hii imehaririwa na MAGRETH KINABO -Mahakama, Dodoma)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni