Jumapili, 13 Aprili 2025

JMAT KUKUTANA MOROGORO, KUCHAGUA VIONGOZI WAPYA

Na ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro.

Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania-JMAT-kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa mwaka mjini hapa kuajdili mambo mbalimbali na kuchagua Viongozi wapya.

Hayo yameelezwa na Rais wa JMAT, ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe John Kahyoza  wakati akizungumza leo tarehe 13, 2025 na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano  huo ambao utafanyika tarehe 15 Aprili, 2025.

Amesema kuwa Chama hicho kina Wanachama zaidi ya 1,500 ambapo kikatiba kila tawi litatuma Wanachama wasiopungua 10.

“Sisi tulichagulia Disemba 2021 na kikomo ilikuwa Disemba 2024, ila tuliahirisha hadi mwezi huu wa Aprili kwa kuwa tulikuwa na Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu Afrika Mashariki, hivyo tusingeweza kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja,” amesema.

Mhe. Kahyoza amesema kuwa  moja ya lengo la JMAT ni kusimamia uhuru wa Majaji na Mahakimu katika utoaji haki pasina kuingiliwa na mamlaka nyingine.

Kwa upande wake,  Katibu Mkuu wa JMAT, Hakimu Mkazi, Mhe. Lazaro Magai amesema kuwa Viongozi watakaochaguliwa ni pamoja na  Rais, Makamu wa Rais, Mweka Hazina, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, huku Katibu Mwenezi akichaguliwa na Baraza Tendaji

“Uchaguzi huu utakuwa wa wazi na Wanachama wapo huru kumchagua mtu wanayemtaka na hatutaraji uchaguzi kwenda kinyume na matakwa ya Wanachama,” alisema Mhe. Magai.

Naye Katibu Mwenezi wa JMAT, Hakimu Mkazi, Mhe. Nimes Michael amesema kuwa mkutano huo utaambatana pia na kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Morogoro ikiwa ni pamoja na maporomoko ya maji choma ndani ya Manispaa ya Morogoro pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

“Mara baada ya mkutano tutaenda kutazama vivutio vyetu vya utalii hapa Morogoro, wapo watakaoenda maporoko ya choma na wengine Hifadhii ya Mikumi, lengo hasa ni kuunga juhudi za Serikali katika kuhamasisha utalii wa ndani na tunaomba Wananchi kuwa na mwamko katika utalii,” alisema Mhe. Nimes.

Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT), Mhe Jaji John Kahyoza (aliyekaa katikati) akizungumza na mkutano na Waandishi wa Habari juu ya mkutano huo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT), Hakimu Mkazi, Mhe. Lazaro Magai akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya mkutano huo.

Katibu Mwenezi wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT), Hakimu Mkazi, Mhe. Nemes Momburi akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya mkutano huo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni