Jumamosi, 12 Aprili 2025

JAJI SARWATT AONGOZA KIKAO CHA KUSUKUMA MASHAURI IJC TEMEKE

  • Wajumbe wadhamiria Mifumo ya Mahakama na Wadau wake kusomana ili kupunguza udanganyifu

Na NAOMI KITONKA, IJC - Temeke

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Sharmillah Sarwatt  amewaongoza Mahakimu na wadau mbalimbali wa Mahakama katika kikao cha Kamati ya kusukuma Mashauri ya Madai (Bench Bar Meeting).

Akizungumza jana tarehe 11 Aprili, 2024 katika ufunguzi wa Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo hicho, Mhe. Sarwatt alisema, “Ni wajibu na jukumu letu kama Mahakama kushirikiana kwa karibu sana na wadau wetu katika utekelezaji wa majukumu yetu na kwa umuhimu huo tunaamini siku ya leo tutapokea mawazo mazuri kutoka kwenu na hiyo itachangia kurahisisha zoezi la upatikanaji haki kwa wananchi tunaowahudumia.”

Alisema kuwa, Kituo Jumuishi Temeke kimelenga kusimamia mpango mkakati wake wa kumaliza mashauri ya mlundikano na kwamba wanatambua umuhimu wa wadau pamoja na vitengo mbalimbali katika kufanya kazi hiyo kwa ukaribu. 

Jaji Sarwatt alisema anaendelea, Mahakama hiyo inajitahidi kuwaalika wahusika na wadau wote ambao majukumu yao yanaathiri utendaji wa kazi ili kupunguza au kumaliza mashauri ya mlundikano.

Aidha, katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wadau walipata wasilisho kutoka kwa Katibu wa Kikao ambaye ni Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Frank Moshi ambapo waliona takwimu za hali ya mashauri kutoka Mahakama Kuu, Mahakama ya Watoto, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo pamoja na sababu zilizochangia mashauri kutokumalizika kwa wakati.

Wadau hao walipata nafasi ya kutoa maoni yao baada ya wasilisho ambapo changamoto kubwa ilionekana ni kuwa na muda mrefu wa kufuatilia mashauri ya mirathi pamoja na kuchelewa kufunga mirathi kwa wakati.

Moja ya majadiliano ilikuwa kuhusu tatizo la vyeti feki vya kifo na kuzaliwa ambapo inaonekana udanganyifu unafanyika kwa kutumia vyeti hivyo ambapo suluhisho lililotolewa ni kuomba mifumo ya Mahakama na wadau wake iweze kusomana ili kuhakikisha taarifa wanazozihitaji zinakuwa siyo za kughushiwa bali ziwe za uhakika.

“Sisi kama ofisi ya RITA tunao utaratibu wetu,  viambatanisho vinavyohitajika ili mteja aweze kukamilisha zoezi la upatikanaji wa cheti cha kuzaliwa au kifo na mara zote wananchi wamekuwa wakikamilisha masharti hayo yote na hivyo kuwa vigumu kujua ni nani anafanya udanganyifu na ofisi imejitahidi kubadili kwa kila namna jinsi vyeti vinavyoonekana ili kupunguza udanganyifu huo kupunguza migogoro,” alisema Afisa Sheria Kutoka RITA, Bi. Janeth Mandawa.

Hata hivyo, ilionekana zoezi la udanganyifu wa kiasi hicho haliwezi kutokea kama hakuna ushirikiano wa mteja na Wakili ambaye anasimamia shauri, hivyo ni muhimu kama Mahakama  kushirikiana kuwatambua Mawakili feki wanaopotosha umma kwa maslahi binafsi na ya wateja wao.

Pia kulikuwa na majadiliano kuhusu kuchelewa kufunga mashauri kutoka Mahakama ya Watoto kuhusu kuchelewa kwa majibu ya vinasaba (DNA) kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kwa upande wa Mahakama Kuu.

Sababu iliyotolewa ni kuwepo kwa amri ya Mahakama ya kufungua shauri upya baada ya makosa kufanyika na pia changamoto ya suala la kubadilisha majina ya umiliki wa ardhi jambo linalosababisha kupita muda wa kusikiliza mashauri uliowekwa kwenye kadi kipimo ambayo ni siku 60 kwa Mahakama ya Mwanzo na Watoto, Siku 90 kwa Mahakama ya Wilaya na Siku 120 kwa Mahakama Kuu.

Akijibu hoja hiyo, Msajili Mkuu wa Hati wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Apolo Laizer alisema, “ni kweli changamoto hii inasababishwa na tatizo la utofauti wa majina ya wahusika na nyaraka za ardhi pamoja na watu wengi kutokuwa na hati za nyumba hali inayosababisha taratibu zingine za kutafuta hati ya kupoteza.

Bw. Laizer alisema pia hati kutoka polisi huchukuliwa katika tangazo la upotevu wa haki na pia zoezi la kubadilisha hufanyika ndani ya siku 30 baada ya kutolewa kwa tangazo la upotevu au kubadilisha hati na kufanya mashauri mengi kufikia hatua ya mlundikano.

Kikao hicho kilihudhuriwa Naibu Msajili, Mhe. Frank Moshi, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Temeke, Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Watoto, Wajumbe wa Sekretarieti kutoka IJC Temeke, Mwakilishi kutoka Chama Cha Mawakili Tanzania (TLS) na wawakilishi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mwakilishi kutoka Benki ya NMB katika Kituo Jumuishi Temeke pamoja na wadau mbalimbali wa huduma za kimahakama kutoka PSSSF, RITA, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hati.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya  Familia Temeke, Mhe. Sharmillah Sarwatt akitoa neno la ufunguzi katika kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika tarehe 11 Aprili, 2025 katika ukumbi wa Mahakama hiyo.

 Naibu Msajili  na Katibu wa Kikao, Mhe. Frank Moshi akitoa ufafanuzi katika kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika jana tarehe 11 Aprili, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho.

Afisa Sheria kutoka Benki ya NMB, Bw. Gilbert Misso akichangia mada katika kikao cha Kusukuma Mashauri  ya Mlundikano kilichofanyika jana tarehe 11 Aprili, 2025 Kituoni hapo.

Afisa Sheria kutoka RITA, Bi. Janeth Mandawa akitoa ufafanuzi wa jambo mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Sharmillah Sarwatt Kazi (hayupo katika picha) kikao cha Kusukuma Mashauri  ya Mlundikano kilichofanyika jana tarehe 11 Aprili, 2025 Kituoni hapo.

Afisa Ardhi Mkuu, Bi. Edith Mganga akimsikiliza kwa makini Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Sharmillah Sarwatt (hayupo katika picha) katika Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Mlundikano kilichofanyika jana tarehe 11 Aprili, 2025 Kituoni hapo.

Msajili wa Hati Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Apolo Laizer akitoa ufafanuzi wa jambo mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Sharmillah Sarwatt Kazi (hayupo katika picha)  katika Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Mlundikano kilichofanyika jana tarehe 11 Aprili, 2025 Kituoni hapo.


Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai ambao ni wadau wa Mahakama kutoka Taasisi mbalimbali wakisikiliza kwa makini wasilisho kutoka kwa Naibu Msajili na Katibu wa Kikao, Mhe. Frank Moshi (hayupo katika picha) alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mashauri ya mlundikano katika kikao hicho kilichofanyika jana tarehe 11 Aprili, 2025 Kituoni hapo.

Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai ambao ni wadau wa Mahakama kutoka Taasisi mbalimbali wakimsikiliza kwa makini Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Sharmillah Sarwatt (aliyekaa mbele) alipokuwa akizungumza jambo katika kikao hicho kilichofanyika jana tarehe 11 Aprili, 2025 Kituoni hapo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni