Jumamosi, 12 Aprili 2025

HAKIMU MKAZI BAGAMOYO AINADI MAHAKAMA YA TANZANIA KIMATAIFA KUHUSU MATUMIZI YA TEHAMA

·       Ni wakati akiwasilisha mada katika Mkutano wa Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) Cape Town

·       Abainisha faida zitokanazo na matumizi ya TEHAMA, mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia

·       Alionesha Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na miundombinu ya TEHAMA iliyopo, washiriki wastaajabishwa

Na MARY GWERA, Mahakama-Cape Town

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mwambao Bagamoyo, Mhe. Edith Mwalukasa ametoa rai kwa Wanachama wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama zana za kulinda haki, kukuza usawa wa kijinsia, kuwezesha upatikanaji wa haki badala ya kuleta madhara.

Mhe. Mwalukasa aliyasema hayo jana tarehe 11 Aprili, 2025 alipokuwa akiwasilisha mada inayohusu Athari za teknolojia kwenye Ukatili wa Kijinsia katika Mkutano wa 17 Chama hicho unaofanyika katika Mji wa Cape Town nchini Afrika Kusini, ambapo ametoa mfano wa Mahakama ya Tanzania kutumia TEHAMA ipasavyo katika jukumu la utoaji haki ikiwemo upatikanaji wa taarifa za kijinsia .

“Sote tukubali matumizi ya Akili Unde (AI) kuhakikisha usawa wa kijinsia, mustakabali wa teknolojia usiwe mustakabali wa ukosefu wa usawa,” alisema Mhe. Mwalukasa.

Alisema kuwa, matumizi ya Akili unde yanaweza kuchanganua mkusanyiko mkubwa wa data na kutambua vipengele vya hatari na mienendo inayohusishwa na vurugu pamoja na kusaidia katika maendeleo ya sera yenye msingi wa ushahidi.

Aliongeza kwamba, Teknolojia inaruhusu upatikanaji wa elimu ambayo inaweza kupinga kanuni hatari za kijinsia na kukuza usawa.

“Matumizi ya TEHAMA huwezesha utaratibu wa kutoa taarifa kwa mamlaka katika mashauri ya kugundua vurugu, ushahidi wa kielektroniki unaotumika kuthibitisha au kukanusha madai, utoaji wa jumbe chanya za kukomesha ukatili wa kijinsia,” alieleza Hakimu huyo.

Alisema kuwa, matumizi ya akili unde huwezesha kutoa taarifa kwa mamlaka katika kesi ya kugundua vurugu; ushahidi wa kielektroniki unaotumika kuthibitisha au kukanusha madai, jumbe chanya wa kukomesha ukatili wa kijinsia

Aliwaeleza washiriki wa Mkutano huo jinsi Mahakama ya Tanzania ilivyopiga hatua katika matumizi ya TEHAMA, ambapo alitaja baadhi ya mifumo ambayo inatumika katika Mhimili huo ambayo ni pamoja na Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS), TanzLII na mingine.

Akizungumzia kuhusu Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mwalukasa alisema jengo hilo lina Chumba maalum cha Kutolea Taarifa mbalimbali za Kimahakama (Judiciary Situation Room).

Aliongeza kuwa, katika kuhakikisha kuwa Mahakama ya Tanzaia inaendelea kutoa haki kwa wananchi ilianzisha Kituo maalum cha Masuala ya Familia Temeke lengo likiwa ni kushughulikia migogoro ya kifamilia ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu wanawake.

“Vilevile Mahakama ya Tanzania tunatumia Mahakama Mtandao ‘Virtual Court”, Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) na kadhalika vyote ni katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati,” alisema Mhe. Mwalukasa.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mwambao Bagamoyo, Mhe. Edith Mwalukasa akitoa mada kuhusu Athari za teknolojia kwenye Ukatili wa Kijinsia jana tarehe 11 Aprili, 2025 katika Mkutano wa 17 Chama hicho unaofanyika katika Mji wa Cape Town nchini Afrika Kusini.


Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mwambao Bagamoyo, Mhe. Edith Mwalukasa akielezea na kuwaonesha washiriki  jinsi Mahakama ya Tanzania ilivyopiga hatua katika Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na maboresho mengine yanayolenga kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.


Washiriki wa Mkutano wakifuatilia wasilisho lililokuwa likitolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mwambao Bagamoyo, Mhe. Edith Mwalukasa (hayupo katika picha).





Picha mbalimbali za matukio ya siku ya tatu (3) ya Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) unaofanyika jijini Cape Town nchini Afrika Kusini.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Cape Town)

























Hakuna maoni:

Chapisha Maoni