Na MWANAIDI MSEKWA na NAOMI KITONKA-Mahakama, Dar es Salaam
Majaji
wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo
tarehe 23 Aprili, 2025 wamekutana jijini Dar es Salaam kushiriki kwenye warsha kwa
ajili ya kujadili na kuzungumzia masuala yanayohusu miliki bunifu (Intellectual
Property).
Warsha
hiyo inayofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Kambarage
Nyerere imefunguliwa na Amiri wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamisi Juma.
Akizungumza
kwenye ufunguzi huo, Mhe. Mwarija ameeleza kuwa lengo la warsha hiyo ni kujenga uwezo ndani ya Mahakama na kusisitiza kujitolea kwa
pamoja kudumisha utawala wa sheria, haki miliki na kuweka haki miliki kama
kichocheo cha nguvu cha uvumbuzi, ubunifu na mabadiliko ya kiuchumi
“Sisi
kama Mahakama tunajihusisha na sheria hasa pale panapokuwa na migogoro
kuhusiana na haki hizo na mpaka sasa maamuzi yetu yameenda WIPO na maamuzi 45
kutoka Mahakama zetu na wametoa baadhi ya muhtasari wa shughuli zao, mfano watu wa BRELA.” ameongea
Mhe. Mwarija.
Pia
amewapongeza BRELA kwa kuendelea kuhusika na usaidizi muhimu katika kukuza mfumo
thabiti na bunifu wa Mali Miliki kwa maslahi ya Taifa na Wanachi kwa
sababu mashauri mengi yanamalizika kwenye
Taasisi hiyo na rufaa chache zinazokuja Mahakama Kuu.
Naye
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani,
Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, akizungumza katika hafla hiyo ameeleza kuwa kuna
umuhimu mkubwa wa Majaji na maafisa wa Mahakama kushiriki mafunzo hayo kwa
sababu Mahakama inayo jukumu la kuelewa masuala ya miliki bunifu na
kudhihirisha kazi zake katika mzunguko wa utatuzi wa migogoro ya miliki bunifu
na kuendana na mageuzi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa BRELA,
Bw. Godfrey Nyaisa alizungumza
kwa kusema, “Lengo la kukutana leo ni kubadilishana uzoefu na Majaji wa Mahakama ya Rufani ili
kuelewa kitu gani hasa,
kama BRELA wanahusika
kwenye masuala ya umiliki na pale mashauri yanapofika mezani kwao inakuwa ni
rahisi katika kuwasaidia kufanya maamuzi.
‘Matarajio yetu ni kwamba elimu hii itasaidia
kutambua na kulinda bunifu za Watanzania
wenzetu kushirikiana na WIPO na ARIPO,” alisema.
Aliongeza
pia kwa kusema mashirika hayo yanajulikana kimataifa na duniani kote ambapo
ubunifu wowote unaowasilishwa unapitiwa kimataifa na sheria zote zinazotumika
zinasaidia kufanya zoezi hilo kikamilifu.
“Kwenye
Mahakama, mashauri ya miliki bunifu
yanaonekana ni machache kwa sababu mashauri mengi yanamalizwa na kutolewa
maamuzi na mengi yanasababishwa na uelewa wa wahusika na hukumu hutolewa, pale
wahusika wakiridhika wengine huamua kunyamaza na ikishindikana shauri hukatiwa
rufaa na kuja Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani,” alisema.
Akizungumza
kwenye ufunguzi huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Tume ya Ushindani (FCC) Bi. Zaytun Kikila alisema “Tume yetu
imeundwa kwa madhumuni ya kuendeleza na kulinda ushindani thabiti katika
biashara na kumlinda mtumiaji dhidi ya mienendo inayohadaa na kutotenda haki
katika uchumi wa soko na lengo kuu ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji,
usambazaji na ugavi wa bidhaa na huduma…
“..Pia tume imekabidhiwa jukumu la
kudhibiti biashara ya bidhaa bandia kwa kutumia Sheria ya Alama za Bidhaa
(Rajamu) Na. 20 ya mwaka 1963 na marekebisho yake na inaitambua Mahakama kama
chombo muhimu katika utekelezaji wa sheria na kuongeza uaminifu kwa wawekezaji.”
Takribani
Majaji wote wa Mahakama ya Rufani wamehudhuria washa hiyo pamoja na Majaji kutoka Kenya, Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani,
Mhe. George Herbert, Naibu Wasajili na Viongozi wengine wa Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni