Jumamosi, 26 Aprili 2025

SERIKALI MTANDAO, MAHAKAMA KUSHIRIKIANA

Na MWANAIDI MSEKWA na NAOMI KITONKA- Mahakama, Dar es Salaam.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imeahidi kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili kuimarisha na kuboresha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji huduma mbalimbali za kimahakama ikiwemo usikilizaji wa mashauri.

Ahadi hiyo imetolewa jana tarehe 25 Aprili, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Bw. Benedict Benny Ndomba alipokuwa anawasilisha mada kuhusu matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa mashauri kwenye Mkutano wa Mwaka wa Mahakama ya Rufani uliokuwa unafanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Julius Nyerere jijini Dar-es-Salaam.

Akizungumza katika wasilisho lake, Bw. Ndomba alisema, “Kila Taifa, sekta na Taasisi ulimwenguni zinalenga mkazo wa matumizi ya TEHAMA ili kuboresha utendaji kazi na kuwahudumia Wadau kwa urahisi na ufanisi.

Aliongeza kwa kusema TEHAMA ina uwezo wa kuleta mapinduzi chanya kwenye utendaji kazi wa Taasisi, ikiwemo ngazi zote za Mahakama kama ilivyo kwa Taasisi nyingine.

Alieleza kuwa Mahakama iwe tayari kukubali mabadiliko yanayoletwa na teknolojia ikiwemo kuendelea kuboresha taratibu zake za utendaji kazi (Business Process re-engineering) na kujifunza namna ya kuendana nayo kama njia bora zaidi ya kukamilisha majukumu ya kimahakama.

Vilevile katika Mkutano huo, Majaji wa Mahakama ya Rufani na wajumbe wengine wote walipata elimu ya jinsi ya kufurahi pale wanapostaafu kutoka kwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Venance Shilingi, ambaye alisisitiza umuhimu wa kujali afya pamoja na malezi ya familia yenye tija ili kupunguza migogoro na mawazo kabla na baada ya kustaafu.

Aidha, Dkt. Shilingi alitoa zawadi kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kwa Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert baada ya wasilisho lake.

Mkutano huo ulihitimishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na ulihudhuriwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani, Msajili Mkuu, Mtendaji Mkuu, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili, Wakurugenzi, Wasaidizi wa Sheria na watumishi wa kada mbalimbali za Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea zawadi ya kitabu kutoka kwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Venance Shilingi katika Mkutano huo.

Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert akipokea zawadi ya kitabu kutoka kwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Venance Shilingi Katika Mkutano huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Serikali Mtandao (eGA), Bw. Benedict Benny Ndomba akitoa mada kwenye mkutano huo.

Wajumbe wa Mkutano wakisikiliza kwa makini wasilisho kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Serikali Mtandao (eGA), Bw. Benedict Benny Ndomba (hayupo pichani) kwenye mkutano huo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni