Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Mkutano wa mwaka wa
mapitio ya shughuli za Mahakama ya Rufani 2024 uiliokuwa unafanyika kwenye
Ukumbi wa Kimataifa Mikutano wa Julius Nyerere jijini hapa kimehitimishwa leo
tarehe 25 Aprili, 2025 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Akizungumza wakati wa
kuhitimisha Mkutano huo, Mhe. Prof. Juma ametangaza kuunda Kamati ya Kuhuisha
Taratibu za Uendeshaji wa Mashauri katika Mahakama ya Rufani -Business process Re-engineering-ili
kuboresha utendaji kazi katika utoaji haki kwa Wananchi.
Ameagiza mwenendo wa
kikao hicho utayarishwe mapema ili kama kuna mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa
kazi yafanyiwe kwa haraka zaidi.
‘Kitu kimoja ambacho
naenda kukifanya ni kuwa na Kamati ya Business Process Re-engineering ili ianze
kazi mara moja na kutupa taarifa kwa muda mfupi ili tujue tunaweza kufanya
nini,’ Jaji Mkuu amesema.
Kabla ya kuhitimisha
Mkutano huo, Wajumbe walipitishwa kwenye mada mbalimbali, ikiwemo matumizi ya
teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA-katika usikilizaji wa mashauri
iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict
Ndomba na Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Kaleghe Enock.
Katika wasilisho lao,
wataalam hao waliwaeleza wajumbe wa Mkutano kuwa matumizi ya TEHAMA katika
sekta na Taasisi mbalimbali hayaepukiki ili kuboresha huduma
kwa urahisi na ufanisi zaidi.
Mada nyingine ilihusu
maandalizi ya kustaafu katika utumishi na uongozi iliyowasilishwa na Mhadhiri Mwandamizi
wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Venance Shilingi pamoja na ile inayohusu namna ya
kuthibiti msongo wa mawazo iliyowasilishwa na Bi. Zuhura Muro.
Katika mada yake, Dkt
Mashillingi amewakumbusha Majaji hao kuwa kustaafu ni fursa ya kuanza maisha
mapya yenye utulivu na furaha, hivyo maandalizi mazuri, yanaweza kuwa na
mchango mkubwa katika jamii na kufurahia maisha.
‘Panga maisha yako: aina
gani ya maisha ungependa uishi? Punguza msongo wa mawazo, usitumie akiba yako
kwa mambo ya siasa. Samehe na kusahau: huu siyo muda wa kuwaza wale
waliokukosea, waliokudhulumu,’ amesema.
Wakati wa Mkutano huo,
wajumbe walipokea na kujadili taarifa mbalimbali zinazohusu mashauri katika
Mahakama ya Rufani pamoja na masuala mbalimbali ya kiutumishi, ikiwa ni pamoja
na ikama, bajeti, stahiki za Majaji, mabadiliko ya sheria kwenye stahiki za
Majaji pamoja na mafunzo kwa watumishi wa Mahakama ya Rufani.
Kadhalika, wajumbe walijadili
masuala mbalimbali katika Mahakama ya Rufani na Mahakama ya Tanzania kwa
ujumla, ambayo yanalenga kuboresha utendaji wa kazi ya utoaji haki.
Mkutano huo ulihudhuriwa
na Majaji wote wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mtandaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Naibu Wasajili, Watendaji na watumishi mbalimbali wa Mahakaka hiyo.
Sehemu nyingine ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Watumishi wengine wa Mahakama-juu na chini-ikiwa kwenye Mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni