Na MARY GWERA, Mahakama-Cape Town
Jumla ya Majaji na Mahakimu Wanawake 43 ambao ni wanachama wa Chama cha
Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wamewasili katika Mji wa Cape Town nchini
Afrika Kusini leo tarehe 08 Aprili, 2025 kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 17 wa
Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani (IAWJ) unaotarajiwa kuanza kesho
tarehe 09 Aprili, 2025.
Akizungumza katika mahojiano maalum leo tarehe 08 Aprili, 2025 mjini
humo, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA),
Mhe. Barke Sehel amesema kuwa, Mkutano huo
unatarajiwa kuanza rasmi kesho tarehe 09 hadi 12 Aprili, 2025 na Mgeni Rasmi
katika mkutano huo anatarajiwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe.
Matamela Cyril Ramaphosa.
“Mkutano huu ni wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Duniani, kwa ujumla unawakutanisha wanachama Majaji na Mahakimu wanawake duniani. Kwa upande wa Tanzania tutakaoshiriki katika Mkutano huo ni wanachama 43 idadi hii imejumuisha na wenzetu wa Zanzibar,” amesema Mhe. Sehel.
Kaulimbiu ya Mkutano huo inasema; ‘Wanawake na uongozi katika
kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya dhidi ya wanawake.’
Mhe. Sehel amesema kuwa, mada mbalimbali zitawasilishwa katika mkutano
huo ni pamoja na Majaji wanawake wanaongoza na kuleta mabadiliko katika Mahakama za
Kimataifa, Wanawake katika Uongozi-Mahali pa Kazi Usalama kwa Maafisa wa
Mahakama, Ubaguzi na biashara haramu ya binadamu na nyingine.
Kwa mujibu wa ratiba ya Mkutano huo, mmoja wa washiriki watakaotoa mada
ya ‘Athari za teknolojia katika masuala ya ukatili wa kijinsia’ ni
Mhe. Edith Mwalukasa ambaye ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mwambao Bagamoyo.
Washiriki wa TAWJA wanaotarajia kuhudhuria mkutano huo ni baadhi ya wanachama ni kutoka kutoka Zanzibar, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Arusha, Tabora na Mikoa mingine ya Tanzania Bara.
Mkutano wa aina hii huwakutanisha pamoja Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani kote na hufanyika kila baada ya miaka miwili na huwapa fursa Majaji hao kujadili masuala mbalimbali yanayohusu haki za wanawake, ukatili wa kijinsia, watoto na jamii kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel akiwa safarini kuelekea mjini Capetown nchini Afrika Kusini kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 17 wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani (IAWJ).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni