Jumanne, 8 Aprili 2025

BARAZA LA WAFANYAKAZI MAHAKAMA KUU MASJALA KUU LAFANYIKA

Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani   leo tarehe 8 Aprili, 2025 amefungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu kujadili mambo mbalimbali ambayo wanakutana nayo kazini.

Baraza hilo limefanyika kikao katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Hoteli ya Rafiki Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Dkt Siyani ambaye ni Mwenyekiti aliwaambia wajumbe kuwa mabaraza hayo ni muhimu kwani yanawapa fursa ya kutoa maoni na ushauri kuhusu nini kinatakiwa kifanyike katika kuboresha mazingira mazuri mahala pakazi.

Kadhalika, Jaji Kiongozi aliwaeleza wajumbe wa Baraza hilo kuwa ili madhumuni ya uwepo wake yatimie, mazingira ya ushiriki na ushirikishwaji wa Wafanyakazi lazima yawe mazuri.

“Kwa Taasisi kama Mahakama, uwepo wa mazingira rafiki yanayowezesha Watumishi kuelewa umuhimu wa Mabaraza ya Wafanyakazi na kudiriki ni muhimu sana,” alisema Dkt.Siyani.

Alisema pia kuwa Viongozi ni lazima waelewe juu ya umuhimu wa kuweka mazingira mazuri yasiyowajengea Watumishi hofu ya kutoa malalamiko, maoni na kushauri.

Jaji Kiongozi alisema kuwa uwezo wa kushiriki na kushirikisha wengine ni sifa muhimu kwa Kiongozi, kwani ukuaji wa Taasisi hautokani na mawazo ya mtu mmoja.

Aliwataka kusimamia maelekezo yote yanayotolewa na Viongozi katika kuhakikisha na kurahisisha kazi kama ambavyo sheria na taratibu zinavyowakataka.

Alimaliza kwa kuwapongeza kwa mafanikio ambayo Mahakama imeendelea kuyapata katika utekelezaji wa jukumu lake la msingi la utoaji haki.

“Ninatarajia kupitia majadiliano katika Baraza hili mtapata fursa ya kuweka mikakati ya kuimarisha zaidi utoaji haki. Baraza hili liwe kioo cha kujitazama na hivyo kurekebisha pale ambapo hatukufanikiwa kama mnavyojua, kwa kufanya hivyo malengo ya uwepo wa Baraza hili yatakuwa yamefikiwa,” alisema Dkt. Siyani.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.Mustapher Siyani akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi la Mahakama Kuu Masjala Kuu lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Rafiki Hoteli uliopo Jijini Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Siyani (aliesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo.
Sehemu ya wajumbe wa kikao hicho wakisikiliza kwa umakini wakati wa kikao hicho.



Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni