Jumanne, 8 Aprili 2025

BARAZA LA WAFANYAKAZI WA MAHAKAMA KANDA YA DAR ES SALAAM LAFANYIKA

Na MWANAIDI MSEKWA-Mahakama, Kazi

Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam hivi karibuni ilifanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji.

Baraza hilo ambalo lilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, liliongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Ngunyale, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo aliwashukuru Viongozi wote waliowezesha kufanyika kwa Baraza hilo.

Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu kinachowakutanisha meza moja Wafanyakazi pamoja na Uongozi ambao ni Mwajiri kwa ajili ya kujadili, kutathimini na kuangalia ustawi wa Wafanyakazi na thamani ya Mfanyakazi na ya yule anaye hudumiwa,’ alisema.

Alieleza pia kuwa Baraza hilo ni muhimu ambalo kila mmoja anahitaji ushiriki wa pekee kwa kutoa maoni na kuhoji ili kuweza kujenga malengo mahususi yanayohusu Wafanyakazi, mazingira ya kazi, nidhamu na kujengeana uwezo.

Mwenyekiti huyo aliwapongeza Watumishi katika ngazi zote za Mahakama, Kanda ya Dar es Salaam kwa kazi nzuri wanazofanya kwani kazi kubwa imefanyika na mafanikio yanaonekana.

‘Changamoto za watu wasio wajibika ni chache sana katika maeneo ya kazi na ambazo zinashughulikiwa kwa ukaribu na kuhakikisha hazileti athari zinazoweza kuleta madhara kwa Wananchi wanaotegemea huduma katika Mahakama,’ Jaji Ngunyale alisema.

Aliwataka kusimamia maelekezo yote yanayotolewa na Viongozi, akiwemo Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na wengine kupitia waraka mbalimbali katika kuhakikisha kazi zinaenda kwa jinsi ilivyopangiliwa.

Jaji Ngunyale alitumia fursa hiyo kuwakumbusha msisitizo wa Jaji Mkuu kuendeleza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA- ili kurahisisha kazi na kuwafikia Wananchi kwa kupitia mifumo iliyopo.

Kufanya hivi inasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri, lengo ni kuhakikisha kuwa Mwananchi hatumii gharama kubwa katika kuendesha kesi yake,’ alisema.

Katika mkutano huo, Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka aliwasilisha taarifa ya utendaji, matumizi ya teknolojia na hali ya miundombinu ya majengo ya Mahakama inayoendelea kuboreshwa.

Naye Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo alielezea hali ya uendeshaji na takwimu za mashauri na kuwahimiza Mahakimu kuongeza kasi ya uondoshaji mashauri na kuongeza jitihada za makusudi katika kila ngazi ya Mahakama ili kufikia malengo ya kitaifa kwa kupunguza au kuondoa kabisa mlundikano.

Kwa kutambua na kuthamini jitihada na mchango wa Watumishi katika utendaji kazi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi alimchagua Bi. Riziki Sakoro, ambaye ni Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Mwanzo Bungu, Wilaya ya Kibiti katika Mkoa wa Pwani, kuwa Mfanyakazi Bora wa Kanda kwa mwaka 2025.

 

Meza Kuu ikiongoza kuimba Wimbo wa Mshikamano, katikati ni Mwenyekiti wa Baraza, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale, aliyeshika kipaza sauti ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi na upande wa kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Pwani Mhe. Joyce Mkhoi.

Wajumbe wakiwa katika kikao.

Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka akiwasilisha taarifa ya utendaji wa shughuli za kimahakama.

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo akielezea hali ya uendeshaji na takwimu za mashauri.

Mfanyakazi Bora Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Riziki Sakoro, ambaye ni Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Mwanzo Bungu, Wilaya ya Kibiti katika Mkoa wa Pwani.



Meza Kuu pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Dar es Salaam -picha mbili juu na picha mbili chini-wakiwa katika picha ya pamoja.



Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro.

 

 

 

 

 

 

  

Maoni 1 :