Na DHILLON UISSO-Mahakama, Ardhi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda, hivi karibuni aliwaongoza Watumishi kufanya
kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha mwaka 2025.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi
wa Wazi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Luvanda aliwaambia Watumishi hao
kuwa Mabaraza hayo ni muhimu kwani yanawapa fursa ya kutoa maoni na ushauri
kuhusu nini kinatakiwa kifanyike katika kuboresha mazingira ya mahala pakazi.
Kadhalika, Jaji Mfawidhi aliwaelezea kuwa vikao vya
mabaraza hayo vinafanyika mara chahe kwa mwaka, hivyo ni muhimu kwa Watumishi kuchangia
Mawazo chanya ili kuboresha maslahi yao.
Akizungumza na wajumbe katika kuchangia hoja ya utawala
na mashauri, Mhe. Luvanda alisisitiza kuwa Chama cha Wafanyakazi ni chombo muhimu
kwa ajili ya kusimamia maslahi mapana ya Wafanyakazi.
Pamoja na hilo, Jaji Mfawidhi alisisitiza Viongozi
wa TUGHE Tawi kushiriki mafunzo mbalimbali ili kuwa mabalozi wazuri kwa
Watumishi wengine kujiunga na Chama hicho kwa maslahi mapana ya kusimamia hoja za Watumishi.
Kiongozi wa TUGHE Tawi la Mahakama Kuu Divisheni ya
Ardhi, Bw. Shaibu Kanyochole alisema kuwa miongoni mwa hoja zilizotolewa na Watumishi
wa Mahakama ni pamoja na kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara kwa ajili ya
kuongeza motisha ili waweze kwenda na mabadiliko ya matumizi ya TEHAMA ambayo
yanajitokeza kwa sasa na kuongezewa vitendea kazi.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa TUGHE
Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Grace Magereli aliwashauri wajumbe kujenga hoja zao
vizuri ili zitakapopelekwa katika Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi Taifa ziweze
kujibiwa vizuri na Viongozi.
Aliendelea
kufafanua na kushauri Watumishi kujiunga kwenye chama kwa lengo la kuwa na nguvu
ya pampoja ili chombo hicho kiweze kuongea kwa nguvu zaidi na kubeba hoja
zitakazopelekwa TUGHE Taifa.
Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi
wameweza kushiriki katika kikao hicho cha kujadili masuala mbalimbali ya
kiutumishi, bajeti na ikiwa ni maandalizi ya Kikao kitakachofanyika Dodoma tarehe
10 na 11 Aprili, 2025.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni
ya Ardhi, Bw. Peter Mbaguli alizitolea ufafanuzi baadhi ya hoja ambazo zinaweza
kutatulika ndani ya Divisheni na kuahidi kuwasilisha kwenye Baraza Kuu hoja ambazo
zitahitaji majibu ya mwajiri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni