Jumatatu, 26 Mei 2025

JAJI MFAWIDHI GEITA ATEMBELEA WAFUNGWA, MAHABUSU GEREZANI

Na DOTTO NKAJA-Mahakama, Geita

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina hivi karibuni alifanya ziara katika Gereza la Geita ili kusikiliza changamoto kutoka kwa Wafungwa na Mahabusu.

Akiwa katika Gereza hilo, Mhe. Mhina alisikiliza changamoto mbalimbali ikiwemo Wafungwa kucheleweshewa nakara za hukumu, vitabu kutotolewa kwa wakati na mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya mtandao kuwa changamoto kwa Wafungwa na Mahabusu.

Changamoto nyingine ni upande wa Jamhuri kuchelewesha kuleta mashahidi kwa wakati na kesi zinazoshushwa kutoka Mahakama ya Rufani kurudishwa Mahakama Kuu kutopangiwa muda wa kusikilizwa kwa wakati.

Akitroa ufafanuzi wa changamoto hizo, Mhe. Mhina alisema changamoto ya mifumo kwa sasa siyo kisingizio cha kuchelewesha kutoa uamuzi katika utoaji haki, bali ni watumiaji wenyewe ndiyo wanaochelewesha kwa kushindwa kufuata utaratibu.

Aidha, aliwahimiza upande wa Jamhuri kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati, hivyo kuondokana na changamoto hizo.

Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Fredirick Lukuna, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Geita, Bi. Masalu Kisasila, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Mhe. Cleofas Wanne, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Geita, Mhe. Salius Muchunguzi na Maofisa kutoka Vyombo vya Dora.



Maofisa wa Gereza la Wilaya ya Geita wakimpokea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina akisaini kitabu cha wageni katika Gereza la Geita.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina-juu na chini- akisikiliza na kutoa ufafanuzi wa changamoto kwa Wafungwa na Mahabusu Wanawake na Wanaume-hawapo kwenye picha- katika Gereza la Wilaya ya Geita.

Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Geita, Afande Lusajo Mwasalyanda akitoa ufafanuzi wa mambo fulani wakati wa ziara hiyo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni