Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Katavi
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama Mhe. Prof.Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji na Mahakimu kuwa na
utayari wa kusikiliza mashauri yanayotokana na Uchaguzi na kutokuwa chanzo cha
ucheleweshwaji wa uamuzi wa mashauri hayo.
Jaji Mkuu ameyasema hayo jana mjini Mpanda wakati
akizungumza na Watumishi wa Mahakama katika ziara ya siku nne ya Makamishna wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
”Huu ni mwaka wa uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani, na kwa mujibu wa Katiba sisi Watumishi wa Mahakama hatutahusika na
shughuli za kisiasa, tutahusika na kupiga kura tu”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema kutokana na uchaguzi huo kutakuwa na mashauri
yatakayofunguliwa hivyo Majaji na Mahakimu wasiwe chanzo cha ucheleweshwaji wa
mashauri hayo yanayotakiwa kuwa yamesikilizwa na kumalizwa ndani ya muda mfupi.
Jaji Mkuu alisema katika mchakato wa shughuli za uchaguzi
Mahakama ya Tanzania imepewa majukumu kwa mujibu wa sheria hasa katika utatuzi
wa migogoro inayotokana na uchaguzi huo. Aliongeza kuwa Sheria ya uchaguzi
iliyotungwa mwaka jana inaonesha kuwa hata Mahakama za Mwanzo zina jukumu la
kutatua baadhi ya migogoro ya uchaguzi.
Aidha, ametoa wito kwa Mahakimu na Naibu Wasajili kuisoma
Sheria ya uchaguzi na kufahamu wamepewa majukumu gani chini ya sheria hiyo
ili mashauri ya uchaguzi yanapofika mbele yao waweze kuyasikiliza na kuyamaliza
kwa haraka.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu wa Tanzania amewataka
Watumishi wa Mahakama kuwa na tabia ya kutaka kujiendeleza kielimu kwa kuwa
Dunia ya sasa inaihitaji mtu kujiongeza mwenyewe kujitafutia maarifa na ujuzi
ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia.
Aidha amewapongeza Watumishi wa Mahakama mkoani Katavi
kwa kutokuwa na mashauri ya Mlundikano ambapo alisema kuwa kukosekana kwa
mshauri ya mlundikano ni dadlili kuwa watumishi wanafanya kazi kwa bidii na
kutoa haki kwa wakati.
Akielezea malengo ya ziara ya Tume katika mkoa huo, Jaji
Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume alisema Tume imefika ili kuwakumbusha
Watumishi hao Kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii na kiuchumi
na pia kuwakumbusha umuhimu wa ushirikiano mzuri kati ya Mhimli wa Serikali na
Mahakama.
Alisema alipozungumza na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.
Mwanamvua Mrindoko alimueleza kuwa kuna uhusiano mzuri kati ya Mahakama na Serikali
mkoani humo na kila upande unaelewa mipaka yake.
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na
ziara ya siku nne katika mikoa ya Katavi na Rukwa yenye lengo la kuziimarisha
Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za mikoa na wilaya ili ziweze kutekeleza
ipasavyo jukumu lake la usimamizi wa maadili na nidhamu ya watumishi wa
Mahakama.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba
kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja
ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili
wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa
wananchi.
Sehemu ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mkoa wa Katavi. Tume imeanza ziara ya kikazi katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni