Jumanne, 27 Mei 2025

JAJI MFAWIDHI TABORA AMUAPISHA MHE. MAGRETH SIMBI KUWA MSULUHISHI WA BARAZA LA USULUHISHI

Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi amemuapisha Mhe. Magreth Simbi kuwa Msuluhishi wa Baraza la Usuluhishi na Uamuzi la mkoani Tabora. 

Hafla ya uapisho ilifanyika jana tarehe 26 Mei, 2025 ofisini kwa Jaji Mfawidhi ambapo mara baada ya kumuapisha Msuluhishi huyo, Mhe. Dkt. Mambi alieleza kuwa kazi ya usuluhishi ni ya kipekee na yenye umuhimu mkubwa katika kudumisha amani na haki katika jamii.

“Kazi ya usuluhishi ni kazi ya kimungu, inahitaji hekima, busara, na uvumilivu wa hali ya juu. Msuluhishi ni mpatanishi mwenye heri na mtendahaki na panapokuwa na haki, amani hutawala.”  Jaji Mambi.

Kwa upande wake, Mhe. Magreth Simbi, mara baada ya kula kiapo alitoa shukrani zake kwa Jaji Mfawidhi kwa nasaha zake na kuahidi kutekeleza kile alichokisikia na kuelekezwa.

“Ninamshukuru sana Jaji Mfawidhi, Mhe.Dkt. Mambi kwa kuniapisha leo, naahidi kutekeleza wajibu huu kwa uadilifu na utiifu kwa msaada wa Mungu. Nitayazingatia yote niliyoelekezwa kwa moyo mmoja,” alisema Mhe. Simbi.

Uapisho huo ni sehemu ya utekelezaji wa Muundo wa Baraza la Uamuzi na Usuluhishi ambao utasaidia ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa njia za usuluhishi. Mbinu hiyo itasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri katika baraza hilo na kujenga utamaduni wa majadiliano ya amani.

Mhe. Simbi ameanza rasmi jukumu lake la kusuluhisha migogoro kwa mujibu wa sheria na kanuni za Kazi. Atahudumu rasmi katika Baraza la Usuluhishi na Uamuzi la mkoani Tabora na atahudumia wananchi wenye migogoro mbalimbali ya kazi. 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akimuapisha rasmi Mhe. Magreth Simbi kuwa Msuluhishi wa Baraza la Usuluhishi na Uamuzi mkoani Tabora.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akimkabidhi nakala ya kiapo Mhe. Magreth Simbi mara baada ya kula kiapo cha kuwa Msuluhishi wa Baraza la Usuluhishi na Uamuzi mkoani Tabora.

Mhe. Magreth Simbi (kushoto) akitoa neno la shukrani kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam  Mambi baada ya kuapishwa rasmi kuanza majukumu ya usuluhishi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akitoa nasaha na maelekezo kwa Mhe. Simbi kuhusu umuhimu wa kazi ya usuluhishi katika kuimarisha haki na amani.

Picha ya pamoja ya kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Jaji Dkt. Adam Juma Mambi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Magreth J. Simbi (kushoto) mara baada ya zoezi la uapisho.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni