Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imepokea rasmi Mahakama Inayotembea, gari la kisasa lenye vifaa vyote vya kisasa kwa ajili ya uendeshaji wa mashauri, ikiwa ni hatua ya kuimarisha utoaji wa haki kwa wananchi wa maeneo ya mbali.
Gari hilo lilipokelewa jana tarehe 26 Mei, 2025 katika viwanja vya Mahakama Kuu Tabora sambamba na kutolewa kwa mafunzo ya siku moja kwa watumishi wa Mahakama kuhusu huduma kwa wateja namna ya kulitumia. Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora yalifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe.Dkt. Adam Mambi ambaye alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi ya kimkakati ndani ya Mahakama ya Tanzania.
"Kupitia Mahakama Inayotembea, tunalenga kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi, hasa wa maeneo yasiyofikika kwa urahisi. Hii ni jitihada ya kuhakikisha inapunguza idadi ya wananchi anayekosa haki kwa sababu ya umbali," alisema Mhe.Dkt. Mambi wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yalitolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi Mashauri-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Moses Betwel Ndelwa na Mhe. Sifa Jacob, Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka katika Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri, Watoa mada hao walieleza kuhusu matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) iliyopo kwenye gari hilo, ikiwemo mfumo wa kurekodi ushahidi kwa njia ya sauti na video, mifumo ya kuhifadhi taarifa na vifaa vya mawasiliano vya kisasa vinavyoweza kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao.
"Gari hili ni chombo kamili cha Mahakama, lina uwezo wa kuendesha shauri kama Mahakama ya kawaida. Linawawezesha Mahakimu na Watendaji kutoa huduma hata katika mazingira ya vijijini ambako hakuna majengo ya mahakama," alifafanua Mhe. Ndelwa.
Mafunzo hayo yalijumuisha viongozi na watendaji mbalimbali wa Mahakama, wakiwemo Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Gabriel Ngaeje, Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Emmanuel Munda, Mahakimu Wakazi Wafawidhi, Mahakimu Wakazi, Maafisa Utumishi, Maafisa Tawala, Wasaidizi wa Kumbukumbu pamoja na Madereva.
"Mafunzo haya yametupa uelewa mpana juu ya matumizi ya Mahakama Inayotembea, ni teknolojia ambayo itasaidia kupunguza mlundikano wa kesi na kuongeza ufanisi," alisema mmoja wa washiriki waliohudhuria mafunzo hayo.
"Kupitia Mahakama hii, tutakuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri kwa haraka, kwa uwazi na bila kikwazo cha umbali, miundombinu, majengo ya Mahakama," alihitimisha Mhe. Sifa Kabisa.
Mahakama Inayotembea inatarajiwa kuanza kutoa huduma rasmi katika Wilaya za Sikonge na Uyui na maeneo mengine ikiwemo Kitunda, Kipili na Nyahua ambayo kwa sasa yanategemea Mahakama ya Mwanzo moja pekee licha ya ukubwa wa Wilaya hiyo. Gari hilo litakuwa msaada mkubwa katika kusogeza huduma kwa wananchi na kuongeza imani yao kwa vyombo vya utoaji haki.
Mahakama inayotembea ni gari maalum lililoandaliwa kwa ajili ya kutoa huduma za kimahakama katika maeneo ambayo hayana miundombinu ya kudumu ya Mahakama. Huduma hii ilianza kama programu ya majaribio katika Mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza. Kufuatia mafanikio yake, huduma hiyo imepanuliwa hadi mikoa mingine ikiwemo Tabora, Dodoma na Mbeya.
Huduma hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania unaolenga kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, kwa gharama nafuu na kwa karibu na wananchi wote ili kuendana na Dira ya Mahakama isemayo; ‘Haki sawa kwa wote na kwa wakati.’
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akifungua mafunzo ya matumizi ya Mahakama Inayotembea yaliyofanyika tarehe 26 Mei, 2025 kwenye ukumbi wa Mahakama hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Mhe. Moses Ndelwa akitoa mada kuhusu uendeshaji wa mashauri kupitia Mahakama Inayotembea (Mobile Court Services).
Washiriki wa mafunzo wakifuatilia kwa makini mada kuhusu matumizi ya Mahakama inayotembea.
Mhe. Sifa Jacob, Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka katika Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri (aliyesimama mbele kushoto) akielezea matumizi ya mifumo mbalimbali ya usimamizi wa mashauri iliyopo katika Mahakama Inayotembea.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya Mahakama Inayotembea wakiwa ndani ya Mahakama hiyo kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni