- Awasihi kusoma Kanuni za Maadili ya Maafisa wa Mahakama na kuziishi
- Awasisitiza pia kuzingatia matumizi ya TEHAMA mahakamani
Na DHILLON JOHN, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 10 Juni, 2025 amewaapisha jumla ya Mahakimu Wakazi wapya tisa na kuwataka kutokuwa chanzo cha migogoro kwa kuchelewesha haki au kutoa haki bila kufuata sheria.
Akizungumza na Mahakimu hao mara baada ya kuwaapisha katika Ofisi ndogo za Jaji Mkuu zilizopo Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, migogoro huweza kusababishwa pia kwa kutofuata ushahidi.
“Nawasihi mkaoneshe tabia njema, uthabiti, uhuru, uwezo ili kutoa haki bila kupendelea na mkifikia kufanya hivyo mtaweza kabisa kujenga jina zuri la Mahakama ya Tanzania,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe. Prof. Juma amewasisitiza Mahakimu hao kusoma kanuni za maadili za Maafisa wa Mahakama ambazo zinapatikana kwenye mifumo ya Mahakama mfano TanzLII na mifumo mingine ya kimahakama ili wazielewe na kuzitekeleza kanuni hizo na kuwasaidia kutopata matatizo kwenye kazi yao ya uhakimu.
“Kanuni hizo utazipata kupitia simu zenu, kompyuta. Mtazipata kwa haraka na kwa wakati kazisomeni kanuni hizo ndio kioo cha Mihimili mingine kujua Hakimu huyu yukoje na kanuni hizo zipo za Mahakimu, Mawakili, Wanasheria wa Serikali na Madalali wa Mahakama, katika kanuni hizo kanuni mbili zinasisitiza Hakimu kutembea nazo saa zote kila wakati katika ufanyaji wako wa kazi,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Pamoja na hayo, Mhe. Prof. Juma amewahimiza kutafuta taarifa bila kusubiri taarifa ziwafikie kwa mfano mabadiliko ya sheria au kanuni ili kutokutoa uamuzi kwa kutumia sheria zilizopitwa na wakati.
Kadhalika, Mhe. Prof. Juma amewasisitiza Mahakimu hao kuzingatia uwezo, weledi, ujuzi wa kitaaluma, uadilifu na uwajibikaji.
Pamoja na hayo, Jaji Mkuu amewaeleza Mahakimu hao wapya kuwa, Mahakama ya Tanzania imetoka katika dunia ya makaratasi na sasa ipo kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa asilimia 100 hivyo amewataka nao kuendana na kasi ya Mahakama katika kuzingatia matumizi hayo.
Amesema kwa sasa Mahakama inaendesha mashauri kwa njia ya TEHAMA na kuwasisitiza wasiikimbie matumizi ya teknolojia bali wakimbilie ili kukuza weledi na kuendeleza taaluma zao kuwa Mahakimu bora na kuja kuwa viongozi wazuri wa baadae.
“Teknolojia haikwepeki na Mhimili wa Mahakama ni nyumbani kwa teknolojia kwa kuwa tumewekeza sana katika mifumo ya teknolojia na tunatarajia kila mtu ataogelea kwenye teknolojia kwakuwa hili ni jambo muhimu sana,” amesisitiza.
Mhe. Prof. Juma ameongeza kwa kuwasisitiza Mahakimu hao kuridhika na kazi ya uhakimu na ujaji huku akiwaeleza kwamba, uhakimu sio utajiri na utajiri wa Jaji na Mahakimu ni hekima, werevu na uadilifu.
“Kama unategemea utajiri kupitia uhakimu basi taaluma hii haikufai bali Jaji na Hakimu ni matajiri wa heshima kwa kazi zao, hiyo ndio furaha yetu kutoa haki na kwa wakati,” amesema Jaji Mkuu.
Mahakimu walioapishwa ni Mhe. Dativa Charles Kiberenge, Radhia Abdallah Luhuna, Mhe. Emmanuel Elinazi Mweta, Mhe. Seth Thomas Mapunda, Mhe. Gibons Joseph Mwaigonela, Mhe. Lucyupendo Valentine Kimaro, Mhe. Mpoki Lusubilo Mwabela, Mhe. Finias Ladslaus Kinigwa na Mhe. Baraka Living Tenga.
Aidha, Hakimu mwingine Mhe. Fraja Thomas Shayo ataapishwa tarehe 11 Juni, 2025.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Herbert George, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, pamoja na Naibu Wasajili waliohudhuria hafla hiyo.
Matukio katika picha hafla ya uapisho wa Mahakimu Wakazi wapya tisa walioapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 10 Juni, 2025 jijini Dar es Salaam.
1.















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni