- Awataka kutenda Haki na Kutunza Siri
Na Arapha Rusheke, Mahakama
Kuu Dodoma.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo
amewaapisha
baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na
ngazi ya Wilaya na kuwataka wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa kutenda
haki.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wajumbe hao tarehe 9, Juni, 2025 katika ukumbi wa Mikutano uliopo Kituo jumuishi cha utoaji haki (IJC) Dodoma, Jaji Mfawidhi pia aliwataka wajumbe wote wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya kutekeleza jukumu lao la msingi la kusimamia maadili ya Mahakimu kwa uaminifu na kwa weledi.
”Tendeni haki mnapotekeleza jukumu lenu la msingi la usimamizi wa maadili na nidhamu ya Mahakimu, muwe na utamaduni wa kutoa nafasi ya kuwasikiliza wale wanaofikishwa mbele ya Kamati zenu ili muweze kutenda haki”, alisema Mhe. Dkt Masabo.
Akizungumzia umuhimu wa
mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili yanayoratibiwa na Sekretariet ya Tume
ya Utumishi wa Mahakama, Dkt Masabo alisema yana umuhimu mkubwa kwa kuwa
yatawajengea uwezo na kuwaimarisha wajumbe katika utekelezaji wa majukumu yao.
Jaji huyo aliwakumbuka
wajumbe umuhimu wa kutunza siri za kamati na kufanya uamuzi wa pamoja
wanapokuwa katika vikao vya kamati. Aliongeza kuwa wajumbe hao hawana budi kuwa
kioo cha wengine kwa kuwa na maadili na nidhamu.
Vilevile Dkt Masabo
alitumia wasaa huo kwa kuwapatia elimu kuhusu kanuni za uendeshaji wa kamati za
maadili ya Maafisa Mahakama ambazo zitawasaidia katika utendaji kazi wao. Aidha,
baada ya kupatiwa mafunzo, wajumbe walionesha kufurahia kitendo hicho cha
kuelimishwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya
Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo Mhe. Rosemary Senyamule amewasisitiza
wajumbe wa Kamati ya Mkoa kukutana na kufanya vikao vya kamati na kuhakikisha
vikao hivyo vinafanyika kwa wakati kwa mujibu wa Sheria. Lakini pia ameipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa maboresho mazuri ambayo yanaendelea kuonekana kwa
Wananchi kwa Ujumla.
Mhe. Senyamule aliwataka
wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa kutekeleza
wajibu wake wa kusimamia maadili na nidhamu ya Mahakimu kwa kufuata taratibu na
Sheria zilizowekwa.
Walioapishwa ni Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule (Mwenyekiti), Wakuu wa wilaya za Dodoma, Chamwino
Ikulu, Kongwa, Mpwapwa, Bahi, Chemba na Kondoa (Wenyeviti) pamoja na wajumbe
wengine wa Kamati ngazi ya Mkoa na wilaya za Mkoa wa Dodoma.
Tume ya Utumishi
wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji
wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya
Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la
msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama,
pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya
Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
Ili
kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya
Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu
cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu
Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya
sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za
Mikoa na Wilaya.
Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya wakiapa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Juliana Masabo tarehe 9 Juni, 2025 jijini Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo(aliyesimama) akizungumza jambo na wajumbe wa kamati za Maadili. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mwenyekiti wa kamati ya maadili ya Maafisa Mahakama Mkoa Mhe Rosemary Senyamule.
Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma Mhe Dkt Juliana Masabo akiwa katika picha ya pamoja na Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama mara baada ya kuwaapisha.
Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma Mhe Dkt Juliana Masabo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi na wageni waliohudhuria uapisho
huo.
(Habari hii imehaririwa na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni