- Yale iliyozoa SHIMIWI, Mei Mosi baada ya kuibuka washindi kwenye michezo mbalimbali
Na
GODFREY KUSOLWA-Mahakama, Dodoma
Timu
ya Michezo ya Mahakama ya Tanzania, Mahakama Sports, jana Jumatano tarehe 11
Juni, 2025 ilikabidhi kwa Uongozi wa Mahakama vikombe 15 ilivyokusanya kwa
vipindi vitatu baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali
iliyofanyika kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za
Serikali-SHIMIWI-na Mei Mosi kuanzia mwaka 2023.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alipokea vikombe hivyo na kutoa medali na vyeti kwa washindi wa michezo mbalimbali katika mashindano hayo. hafla hiyo ilifanyika kwenye moja ya Kumbi za Mikutano katika Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma,
Akizungumza
katika hafla hiyo, Prof. Ole Gabriel aliwapongeza wanamichezo hao walioweza
kushiriki na kuibuka washindi kwenye michezo ya SHIMIWI iliyofanyika katika
Mikoa ya Iringa na Morogoro na mashindano ya Mei Mosi yaliyofanyika katika Mikoa ya Arusha na
Morogoro na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza michezo
hapa nchini.
Akizungumzia
mipango ya kuwekeza katika kutambua vipaji vya michezo ndani ya Mahakama ya
Tanzania, Mtendaji Mkuu aliuliza, “Hivi hatuwezi siku moja tukacheza na Timu za
Simba au Yanga pale kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa?”
Aliongeza,
“Maono yangu, ni kuona siku moja tunapata timu bora za kushiriki kwenye
michuano mbalimbali mikubwa ikiwemo mchezo wa riadha, na mimi mwenyewe napenda
kucheza mchezo wa vishale, yaani (Darts).”
Prof.
Ole Gabriel aliwaambia wanamichezo hao kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahimu Hamis Juma, siku zote amekuwa muumini wa michezo kwani anaamini michezo
ni uchumi na inaweza kumuongezea mtu kipato binafsi na kuchangia katika pato la
Taifa kwa ujumla.
MtendajiMkuu
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi za
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani
na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya kwa mafanikio
makubwa ambayo wanamichezo hao wameyapata.
“Uongozi
wote wa Mahakama ya Tanzania unatambua umuhimu wa mashindano hayo kwa Watumishi
wa Umma, ikiwemo wa Mahakama. Nakubali kutoa wiki moja kwa washiriki kujiandaa
kabla ya mashindano, maana hilo naliweza,” alisema.
Naye
Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede, akizungumza katika hafla hiyo,
aliushukuru uongozi kwa hatua inazochukua kuhakikisha wanashiriki kwenye
mashindano mbalimbali.
Baadhi ya Washindi katika mashindano hayo walielezea siri ya mafanikio kwenye michezo kama hiyo kama vile kuzingatia nidhamu, programu ya mazoezi na kujituma kupambania Taasisi wakati wote.



















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni