Na Christopher Msagati - Mahakama, Manyara
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza amesisitiza kukamilishwa
miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama kwa wakati ambayo yanaendelea kujengwa kwa
sasa na Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara.
Mhe.
Kahyoza ameyasema hayo wakati akiwa katika ziara ya Ukaguzi wa Mahakama za
Wilaya ya Kiteto na Simanjiro iliyofanyika kuanzia tarehe 12 Juni 2025 hadi
tarehe 13 Juni 2025.
Katika
ziara hiyo Mhe. Kahyoza aliambatana na viongozi mbalimbali waliyoshiriki
Ukaguzi wa maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Kiteto,
Gereza la Wilaya ya Kiteto, Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro pamoja na miradi ya
ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro na Mahakama ya Mwanzo Terrat iliyopo
Wilayani Simanjiro ambayo inaendelea kwa sasa.
Akiwa
katika Ukaguzi wa miradi ya Ujenzi wa Mahakama inayoendelea Wilayani Simanjiro,
Mhe. Kahyoza aliwaambia Wakandarasi wahakikishe kuwa miradi hiyo ya Mahakama
inakamilika mapema kwa sababu shughuli za kimahakama zinatakiwa kuanza ili
wananchi wapate huduma zinazohitajika katika maeneo yao.
“Nawasihi
mjitahidi kumaliza ujenzi huu mapema iwezekanavyo kwa sababu tunapaswa kuanza
kuwahudumia wananchi wa Wilayani Simanjiro vilevile watumishi wa Mahakama hii
wapate jengo bora zaidi kwa sababu sasa wanatumia jengo la kuazima ambalo ni
dogo na halitoshi kwa mahitaji ya Mahakama na pia tuwasaidie wananchi wa Terrat
waweze kupata huduma za kimahakama ambazo kwa sasa wanachelewa kuzipata kwa
sababu inawapasa kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa Hamsini ili kupata huduma
hizo” alisema Mhe. Kahyoza.
Naye,
Mhandisi Samwel James kutoka Kampuni ya Moladi Tanzania Ltd ambayo inajenga
jengo la Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro aliuahidi uongozi wa Mahakama Kuu
Kanda ya Manyara kujitahidi kukamilisha ujenzi huo mapema kwa kuwa wamepata
vifaa vya ujenzi ambavyo vitafanya shughuli yao kufika mbali.
“Kwa
sasa tuna vifaa vya kutosha pamoja na nguvu kazi ya kutosha, hivyo naahidi
kukamilisha ujenzi huu mapema iwezekanavyo” alisema Mhandisi James.
Aidha,
katika upande wa Ukaguzi wa Mahakama zinazofanya kazi kwa sasa, Naibu Msajili
wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo aliwasihi watumishi
kutumia mifumo ya TEHAMA ambayo inatumiwa na Mahakama inarahisisha taarifa
kufika kwa haraka kwa wadaawa na pia inasaidia Ofisi kupunguza matumizi ya
makaratasi na gharama nyingine za uchapishaji.
“Tukiitumia
hii mifumo itatusaidia sana kufikisha taarifa kwa wadaawa wetu mapema zaidi
lakini pia na sisi kama Ofisi tunapunguza gharama za uchapishaji wa nyaraka
mbalimbali na hivyo kuweza kusaidia kupata fedha za kufanya mambo mengine ya
kimaendeleo,” alisema Mhe. Mpepo.
Mahakama
Kuu Kanda ya Manyara inaendelea na zoezi la Ukaguzi wa Mahakama za chini kwa
Robo Mwaka ya kuanzia Mwezi Aprili hadi Juni 2025 kwa lengo la kuangalia
ufanisi na utendaji kazi pamoja na kutoa maelekezo kwa watumishi wa Mahakama ambayo
yatasaidia katika utoaji huduma ya haki kwa wakati.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza akisalimiana na Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto alipofika Mahakamani hapo kwa ajili ya Ukaguzi.
1 Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto Mhe Boniface Lihamwike akisoma
taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wilaya hiyo kwa Mhe. John Kahyoza (hayupo
pichani) ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza akiwa katika picha
ya Pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto, aliyekaa
upande wa Kushoto Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya
Manyara Mhe. Bernard Mpepo na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama
Kuu Kanda ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemed.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (wa pili kulia) akiwa na baadhi ya watu aliombatana nao katika
ziara ya Ukaguzi katika Gereza la Wilaya ya Kiteto.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza akisalimiana na baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro alipofika Mahakamani
hapo kwa ajili ya Ukaguzi.
1. Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (hayupo pichani) wakati
akizungumza nao katika ziara ya Ukaguzi katika Wilaya hiyo.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (kushoto) akizungumza na
baadhi wa wawakilishi wa Kampuni ya Pioneer Builders Company Ltd wanashughulikia ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Terrat iliyopo Wilayani Simanjiro.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni