Ijumaa, 20 Juni 2025

JAJI MWAKAPEJE AKAGUA SHUGHULI ZA KIMAHAKAMA WILAYANI CHATO

 Na DOTTO NKAJA-Mahakama, GEITA

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje hivi majuzi alifanya ukaguzi katika Mahakama ya Wilaya Chato na Mahakama za Mwanzo Nyamirembe na Buseresere na kuonesha kufurahishwa na utekelezaji wa maagizo ya Viongozi, ikiwemo kuzuia na kutrokuzalisha mlundikano wa mashauri.

Mahakama ya Wilaya Chato imefanikiwa kuzuia na kuhakikisha haizalishi mlundikano wa mashauri na kufanikiwa kumaliza mashauri yote yaliyofunguliwa mwaka 2024. Mhe. Mwakapeje alimpongeza Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Amalia Mushi kwa kusimamia na kuratibu vizuri shughuli za Mahakama.

Wakati wa ziara hiyo ambayo aliambatana na Naibu Msajili, Mtendaji wa Mahakama na maofisa wengine, Mhe. Mwakapeje alitembelea pia mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Muganza na kuonesha kutokufurahishwa na kasi kwani hatua ya jengo iliyopo haiendani na muda wa kumaliza jengo hilo.

Kutokana na hali hiyo, alimtaka Mkandarasi kukamilisha ujenzi huo kwa muda kwa sababu jengo hilo linahitajika kwa haraka, ukizingatie kuwa shughuli za kimahakama za Mahakama ya Mwanzo Muganza zinafanyikia kwenye soko.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Geita, Mhe. Fredrick Lukuna aliungana na Jaji Mwakapeje, kwa kuwapongeza Watumishi na Mahakimu wanaofanya kazi katika Mahakama ya Wilaya Chato na Mahakama zake za Mwanzo kwa kufanya vizuri katika uendeshaji wa mashauri.

Pongezi hizo pia ziliungwa mkono na Mtendaji wa Mahakama Kuu Geita, Bi, Masalu Kisasila, aliyewahimiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kufuata maadili ya kazi.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje akisaini kitabu cha wageni katika Mahakama ya Mwanzo Buseresere wilayani Chato.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje akikagua mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Muganza na kuwataka wakandarasi waongeze nguvu ili jengo hilo lianze kutumika.


Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyamirembe, Mhe. Tyson Bashaya akiwasilisha taarifa fupi ya hali ya mashauri pamoja na ya utawala na rasilimaliwatu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje-wa tatu kushoto  akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Buseresere Wilayani Chato.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni