Ijumaa, 20 Juni 2025

WAFUNGWA, MAHABUSU GEREZA KUU LA KARANGA MOSHI WAIPONGEZA MAHAKAMA KANDA YA MOSHI

Wawashukuru watumishi wa Mahakama kwa kujali utu na kuwa na lugha zenye stara wakati wote wanapohudumia wananchi

Wasifu hatua ya kupatiwa nakala za hukumu na mienendo kwa wakati 

Wakoshwa na uendeshaji wa mashauri kwa Mahakama Mtandao

Na PAUL PASCAL, Mahakama -Moshi

Mmoja wa Viongozi wa wafungwa na mahabusu wa Gereza Kuu la Karanga amewapongeza watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi kwa kuwa waungwana na wanaojali utu na kuheshimu watu wote wanaofika kupata huduma katika Mahakama hiyo.

“Binafsi niwapongeze watumishi wa Mahakama Kuu Moshi kwa utoaji huduma nzuri pasipo kujali kuwa ni mtuhumimiwa kwa kweli enzi hizi ukifika Mahakamani unasemeshwa vizuri na unahudumiwa ipasavyo na kwa wakati hakuna mambo ya longolongo tena,” amesema Kiongozi huyo wakati walipotembelewa na Viongozi kutoka Mahakama na wadau wa Haki Jinai  waliofika katika gereza hilo kwa ziara ya ukaguzi.

Aidha, Kiongozi huyo aliuomba uongozi wa Mahakama Kanda ya Moshi kuongeza idadi ya vikao ili kuondokana na kukaa mahabusu na hatimaye siku moja iwe walioko magerezani ni wafungwa tu na sio mahabusu.

Akitoa salamu za ukaribisho pamoja na kusoma taarifa fupi ya Gereza Kuu la Karanga Moshi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Godbless Moshi aliwashukuru Viongozi kutoka Mahakama hiyo kwa kutembelea Gereza hilo.

“Napenda kuwashukuru Mhe. ‘Jaji’ na wote mlioongozana nao nipende kukujulisha kuwa mpaka kufikia tarehe 19 Juni, 2025 tuna jumla ya wafungwa na mahabusu 791 na gereza letu lina uwezo wa kubeba wafungwa na mahabusu 1,200,” alisema Mrakibu Moshi.

Alisema, kati ya idadi hiyo ya 791 wafungwa ni 498 wanaume wakiwa ni 470 na wanawake 28 huku mahabusu ni 293 wanaume ni 277 na wanawake ni 16.

“Kwa takwimu hizi nikiri mbele yako gereza letu linamudu kuwahudumia wananchi hawa kipekee niwapongeze kwa kasi ya umalizaji mashauri pamoja na kuwa na utaratibu mzuri wa dhamana. Mambo haya ndio yametusaidia kupunguza mlundikano wa mahabusu katika gereza letu hakika mnastahili pongezi nikuombe pongezi hizi unifikishie kwa Mhe. Dkt. Lillian Mongella, Jaji Mfawidhi kwani katika kipindi cha uongozi wake tumeona mabadiliko haswa kasi ya umalizwaji mashauri katika Mahakama zote hongereni sana,” alisisitiza.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Safina Simfukwe aliwaeleza mahabusu na wafungwa wa gereza hilo kuwa, lengo la kutembelea gereza hilo ni kuwajulia hali, kuona mazingira pamoja na kujadiliana endapo kuna kikwazo chochote katika majukumu hatimaye kuambiana mambo yote yanayoonekana kama kikwazo katika zoezi zima la upatikanaji haki.

“Ndugu zangu kwanza niwape pole kwa haya yote mnayoyapitia pia niwatie moyo kwa kuwa yote haya ni sehemu ya mapito ya maisha yetu sisi wanadamu niwajuze tu tuko pamoja nanyi kwa wakati wote ndio maana leo tumeona ni vema kufika mbele yenu tukiambatana safu nzima ya wahusika katika mnyororo wa utoaji haki jinai ili tuweze kuwajulia hali, kuona mazingira yenu huku pamoja na kujadiliana endapo kuna kikwazo chochote katika majukumu yetu niwaombe tuambizane mambo yote tunayoyaona kama kikwazo kwenu katika zoezi zima la upatikanaji haki,” alisema Mhe. Simfukwe.

Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ilifanya ukaguzi katika Gereza Kuu la Karanga Moshi jana tarehe 19 Juni, 2025 ikiwa ni ukaguzi kwa robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Ukaguzi huo ambao ulilenga kukagua mazingira ya wafungwa na mahabusu wawapo gerezani pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.

Ukaguzi huo ulioongozwa na Mhe. Safina Simfukwe, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi akiambatana na Naibu Msajili, Mhe. Dkt. Cassian Mshomba, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Mhe Ally Mkama, Mahakimu Wakazi Wafawidhi Wilaya ya Moshi, Siha na Hai, Mahakimu Wafawidhi Mahakama za Mwanzo, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro (RCO), Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro, Mwakilishi kutoka Chama cha Wanasheria wa Kujitegemea (TLS) chapta ya Kilimanjaro, na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kilimanjaro.

Ukaguzi huu ni ukaguzi wa kawaida kwa mujibu wa miongozo ya ukaguzi kwa Mahakama ya Tanzania na ulilenga kuona mazingira na kutatua changamoto zinazowakibili wafungwa katika Gereza Kuu la karanga ambalo linahudumia Wilaya tatu za Kimahakama Kanda ya Moshi ambazo ni Siha, Hai na Moshi.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Safina Simfukwe  (katikati) akiwa pamoja na wadau wa Mahakama katika mnyororo haki Jinai walipofanya ukaguzi katika Gereza Kuu la Karanga-Moshi jana tarehe 19 Juni, 2025. 

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi na K
aimu Mkuu wa Gereza Kuu la Karanga, Godbless Moshi (wa pili kushoto) akimshukuru Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Safina Simfukwe kwa niaba ya wadau wote waliofika kutembelea na kukagua Gereza Kuu la Karanga.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni