Na ASHA JUMA- Mahakama Morogoro
Wizara ya Mambo ya Ndani, kwa kushirikiana na Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro imeendesha mafunzo maalum juu ya utekelezaji wa adhabu mbadala kwa ajili ya ustawi wa Taifa.
Mafunzo hayo yamefanyika jana tarehe 19 Juni, 2025 katika Ukumbi wa Magadu Hotel Morogoro na yalifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Mhe. Musa Kilakala.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa kitaifa unolenga kuwajengea uwezo wadau wa haki jinai katika maeneo mbalimbali nchini ili kukuza matumizi ya adhabu mbadala kama njia ya kupunguza msongamano magerezani na kuimarisha urejeshaji wa wahalifu katika jamii.
Aidha, mafunzo hayo yametolewa kwa lengo la kujenga uelewa mpana juu ya sheria na kanuni zinazo simamia adhabu mbadala Tanzania, kufahamu faida za utoaji wa adhabu za huduma kwa jamii kwa maendeleo ya taifa, kujadili changamoto za utekelezaji wa sheria na mapendekezo ya utatuzi wake na kuongezeka kasi ya utoaji wa adhabu mbadala.
Washiriki wa mafunzo hayo walijumuisha Majaji na Mahakimu kutoka Mahakama Kanda ya Morogoro, wakiongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Rose Ebrahim. Walikuwepo pia Maofisa wa Magereza, uangalizi wa jamii, wawakilishi wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Jeshi la Polisi (NPS) na Wadau wengine muhimu wa haki jinai.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii, pamoja na Bw. Ahmed Mwen-dadi na wengine.
Miongoni mwa mada zilizotolewa ni pamoja na Sheria na kanuni zinazosimamia utoaji na utekelezaji wa adhabu mbadala Tanzania, Sheria ya kifungo cha nje, Utaratibu wa uandaaji wa taarifa ya uchunguzi, Faida za utekelezaji wa adhabu mbadala na Wajibu wa Ofisa Uangalizi katika utekelezaji wa huduma kwa jamii.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mhe. Ebrahim aliwaasa Majaji pamoja na Mahakimu juu ya matumizi ya adhabu mbadala ili kupumguza idadi kubwa ya watu gerezani pamoja na kujenga familia bora, kwani mfungwa atakua karibu na familia yake na kulea Watoto na mwenza wake.
“Tujitahidini sana kuitekeleza sheria hii ya adhabu mbadala kwani inafaida kwa jamii haswa kwenye malezi ya Watoto na husaidia mfungwa anakua karibu zaidi na familia yake , ” alisisitiza.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe.MStephen Magoiga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii akitoa elimu kwa Wadau wa haki jinai.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim akitoa hotuba ya kufunga
mafunzo kwa Wadau wa haki jinai.
Wadau mbalimbali
wa haki jinai wakifatilia mafunzo-juu na chini.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Musa Kilakala (katikati) akiwa katika Picha ya pamoja ya Wadau wa haki jinai na watoaji wa mafunzo ya Sheria na kanuni za adhabu mbadala Tanzania.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni