Jumanne, 24 Juni 2025

MAHAKIMU KIGOMA WAPONGEZWA KUONDOSHA MASHAURI KWA WAKATI

  • Waazimia kumaliza mashauri kwa muda mfupi kabla ya kuwa mlundikano mahakamani

 Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Mwendesha Mashataka Mfawidhi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Kigoma, Bw. Waziri Mbwana Mgumbo amewapongeza Mahakimu wa Wilaya Kigoma kwa kazi kubwa ya kusikiliza na kuamua mashauri kwa wakati.

Bw. Mbwana alisema hayo katika kikao cha kusukuma mashauri ya jinai kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma tarehe 20 Juni, 2025 na kuoongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo.

Mwendesha Mashtaka huyo Mfawidhi alisema kuwa, Ofisi ya Taifa ya Mashataka imejipanga vema kuhakikisha inaisaidia Mahakama kuondosha mashauri yake kwa muda uliopangwa na kuhakikisha mashauri yote yanayosimamiwa na ofisi hiyo yanamalizika kwa muda uliopangwa na Mahakama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo alisema kuwa, Mahakama inategemea uwajibikaji wa wadau wake ili kuharakisha utoaji haki kwa wakati.

Aidha, Mhe. Tarimo alilitaka jukwaa la Mawakili wa Kujitegemea Tanganyika (TLS) kuongeza Mawakili katika umoja wao mkoani Kigoma ili kuongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri  kwa Mahakama za Wilaya za mkoani Kigoma.

Alisisitiza kuwa, “Mahakama inatambua  juhudi kubwa za Mahakimu na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Kigoma pamoja na wadau wote wa Mahakama kwa kufanikisha umalizwaji wa mashauri 45 kabla ya kuwa mlundikano katika robo mwaka iliyopita.” 

Aidha, aliwataka Mahakimu wa Wilaya kuzingatia umri wa mashauri yaliyopo katika Mahakama zao ikiwa ni moja ya mikakati ya kuzuia mlundikano wa mashauri mahakamani.

Alisisitiza kuwa, wadau wote wasipende ahirisho la mashauri mahakamani kwa sababu zisizo za msingi katika kuisaidia Mahakama kutunza muda wake wakuondosha shauri mahakamani ili kuepuka mashauri mlundikano.

Katika kikao hicho Mahakimu wameazimia kumaliza mashauri kwa muda mfupi kabla ya kuwa mlundikano mahakamani.

Wadau walioshiriki kwenye kikao hicho ni pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa, Mahakimu wa Mahakama za Wilaya Kigoma, Kibondo, Kasulu, Uvinza, Buhigwe na Kakonko.

Wengine ni kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Ofisi ya Huduma kwa Jamii, Ofisi ya Upelelezi Mkoa, Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa (TAKUKURU), Ofisi ya Uhamiaji Mkoa na Magereza Mkoa wa Kigoma.

Wajumbe wa kikao cha kusukuma mashauri ya jinai ngazi ya Mkoa wa Kigoma wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Mwenyekiti wa kikao hicho, ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo (aliyeketi mbele kulia).

Sehemu ya wajumbe wa kikao cha wadau wa kusukuma mashauri ya jinai ngazi ya Mkoa, wakifuatilia kwa makini mjadala uliokuwa ukiendelea katika kikao wadau wa haki jinai kilicofanyika tarehe 20 Juni, 2025.

Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Kigoma, Bw. Waziri Mbwana akifafanua jambo wakati wa kikao cha wadau wa kusukumu mashauri ya jinai ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo
  akisisitiza jambo wakati wa kikao cha wadau wa kusukuma mashauri cha mkoa huo kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Mhe. Venance Mwakitalu akifuatilia kwa makini mjadala uliokuwa ukiendelea katika kikao cha wadau wa haki jinai ngazi ya Mkoa kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)

 

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni