Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya
Kigoma, Mhe. John Nkwabi amefungua rasmi
mafunzo maalum kuhusu Kuepuka Kutonesha
Majeraha kwa Waathirika na Mashahidi wa Ukatili wa Kijinsia na Kingono (SGBV).
Mafunzo hayo ya siku tatu, yanayoanza kufanyika
kuanzia tarehe 24 hadi 26 Juni, 2025 katika Mahakama
Kuu Kigoma, yamewakutanisha
jumla ya washiriki 18 wakiwemo Mahakimu
Wakazi, Waendesha Mashtaka, na Maafisa Ustawi wa Jamii.
Akifungua mafunzo hayo, Mhe. Nkwabi alisisitiza kuwa, ni muhimu kutumia lugha yenye huruma, staha na weledi
mkubwa, pamoja na kujenga mazingira ya kimahakama yenye usalama kwa waathirika
wa ukatili huo.
Kadhalika,
Jaji Nkwabi aliwahimiza
washiriki kuwa makini na mbinu wanazotumia katika kushughulikia mashahidi walio
katika mazingira magumu ili wasiwajengee hali ya woga au kukumbuka majeraha yao
ya awali.
“Mafunzo haya yatagusa maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo: Uelewa wa athari za
kiakili na kihisia kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, Mbinu rafiki na
salama za kuwauliza maswali mashahidi wa aina hiyo, Ushirikiano baina ya
taasisi katika kusaidia mashahidi walioko katika mazingira magumu na Mizania ya
kulinda haki za waathirika sambamba na zile za watuhumiwa,” alisema Mhe.
Nkwabi.
Washiriki wa
mafunzo hayo watapata fursa ya
kujadili matukio halisi, kushiriki mazoezi ya vitendo na kuibua maeneo
yanayohitaji maboresho ya kitaasisi. Msistizo na mkazo vimewekwa
katika kujifunza kwa pamoja na kuandaa mikakati ya utekelezaji wa maarifa
watakayoyapata kazini.
Mafunzo haya ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania za kuboresha mifumo ya utoaji haki
ili iwe jumuishi, yenye huruma, na inayowajali wahitaji wa huduma za haki hasa
kutoka makundi yaliyo hatarini.
Mafunzo hayo ni ya awamu ya nne ya mwendelezo wa mafunzo kama hayo ambayo yamefanyika katika mikoa ya Tanga, hususani Wilaya ya Lushoto, Dodoma na Dar es Salaam. Sambamba na mkoani Kigoma napo Songea mkoani Ruvuma yameandaliwa mafunzo hayo na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na ‘Irish Rule’ of Law International (IRLI) na kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)
na IRLI wanatarajia kufanya
tathmini ya utekelezaji wa mafunzo hayo ili kupima mafanikio yake na kuchangia
maboresho ya muda mrefu katika upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukatili wa
kijinsia na kingono.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi akifungua rasmi mafunzo maalum kuhusu Kuepuka Kutonesha Majeraha kwa Waathirika na Mashahidi wa Ukatili wa Kijinsia na Kingono (SGBV) katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma.
Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Bi. Gloria Shuma akitoa neno la utangulizi kwa Mgeni rasmi na washiriki wa mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo maalum kuhusu Kuepuka Kutonesha Majeraha kwa Waathirika na Mashahidi wa Ukatili wa Kijinsia na Kingono (SGBV) wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, (katikati) akimtambulisha Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo (kulia) kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi.
Meza kuu ikiongozwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo (waliosimama) kuhusu Kuepuka Kutonesha Majeraha kwa Waathirika na Mashahidi wa Ukatili wa Kijinsia na Kingono (SGBV). Wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo, wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Mhakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, na wa kwanza kulia ni Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Bi. Gloria Shuma na wa kwanza kushoto ni Afisa Ustawi wa Jamii, Bi Roseana Philemon.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni