Jumatano, 25 Juni 2025

MAHAKAMA SONGEA YAENDESHA MAFUNZO KUHUSU UKATILI KIJINSIA, KINGONO

Na NOEL SYLIVESTER-Mahakama, Songea

Mahakama Kanda ya Songea inaendesha mafunzo maalum kuwajengea uelewa Mahakimi na Wadau mbalimbali kuhusu kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika na mashahidi wa ukatili wa kijinsia na kingono.

Mafunzo hayo ya siku tatu yalifunguliwa jana tarehe 24 Juni, 2025 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha, yakikutanisha Mahakimu Wakazi, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi wa Jamii.

Mafunzo hayo ni endelevu, yakiwa yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Irish Rule of Law International (IRLI), kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo washiriki katika kushughulikia mashauri ya ukatili wa kijinsia kwa kuzingatia athari za kiakili na kihisia kwa waathirika, sambamba na kuheshimu haki za watuhumiwa.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Karayemaha alisisitiza Wanasheria, Polisi na Mahakama kuwatendea ubinadamu na heshima waathirika wanapofikishwa mbele yao na kuheshimu waathirika wa ngono na unyanyasaji kijinsia pale kesi au mashauri yanapofikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe Victoria Nongwa pamoja na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Momba, Mhe. Raymond Kaswaga.  Wapo pia waratibu wa mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mahakama Kuu, Kanda ya Songea, Mhe. Goodluck Ndimbo pamoja na Patric Lipiki kutoka IJA ambao ndio watakaoongoza washiriki kupitia mijadala na mafunzo ya vitendo yenye kuhusisha uzoefu wa kiutendaji.

Mafunzo haya yatagusa maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo: uelewa wa athari za kiakili na kihisia kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, mbinu rafiki na salama za kuwauliza maswali mashahidi wa aina hiyo, ushirikiano baina ya Taasisi katika kusaidia mashahidi waliopo katika mazingira magumu na mizania ya kulinda haki za waathirika sambamba na zile za watuhumiwa.

Washiriki watapata fursa ya kujadili matukio halisi, kushiriki mazoezi ya vitendo, na kuibua maeneo yanayohitaji uboreshaji wa kitaasisi, kujifunza kwa pamoja na kuandaa mikakati ya utekelezaji wa maarifa watakayoyapata kazini.

Mafunzo hayo yamekuwa sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania kuboresha mifumo ya utoaji haki ili iwe jumuishi, yenye huruma na inayowajali wahitaji wa huduma za haki, hasa kutoka makundi yaliyo hatarini.

Chuo cha IJA na IRLI wanatarajia kufanya tathimini ya utekelezaji wa mafunzo hayo ili kupima mafanikio yake na kuchangia uboreshaji wa muda mrefu katika upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na kingono.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa mafunzo.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe Victoria Nongwa akiwa katika uwezeshaji wa mafunzo.


Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Momba, Mhe. Raymond Kaswaga akiwa katika uwezeshaji wa mafunzo.


Sehemu ya wawakilishi wakifuatilia mafunzo hayo.


Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni